Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa CC Mary Chatanda ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha inashughulikia changamoto za ndovu waliovamia makazi ya watu Mkoani Lindi.
Ameyasema hayo leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Naipingo Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi.
Amefafanua kuwa ndovu hao wamevamia makazi ya watu kutokana na wananchi kuingia katika maeneo ya Hifadhi.
"Wizara ya Maliasili Utalii shirikianeni na Wizara ya Mifugo muwatoe wafugaji walioingia kwenye maeneo ambayo ndovu wanakaa" Chatanda amesisitiza
Ameelekeza hatua za haraka zichukuliwe kuwatoa wananchi katika hifadhi ili kunusuru mazao ya wananchi yanayoliwa na ndovu pamoja na vifo vya wananchi.
Kufuatia hoja hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja ameahidi Wizara ya Maliasili na Utalii kupeleka helikopta ya kufukuza ndovu ambayo itaweka kambi katika maeneo husika.
"Tutahakikisha tunaleta helikopta ambayo itakaa kuondoa ndovu hawa ili wananchi waishi bila taharuki" Mhe. Masanja amesisitiza.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inajua Changamoto zinazowakabili wananchi hivyo imepanga kuongeza idadi ya askari na kujenga vituo vya askari ili kuondokana na tatizo la ndovu.
Kuhusu malipo ya kifuta jasho/machozi, Mhe. Masanja amesema Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 612 kwa Wilaya ya Nachingwea mwaka ili kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan ndovu.
Pia amesema Serikali itachukua vijana kwenye maeneo yenye changamoto za ndovu na kuwapatia mafunzo ya kukabiliana na wanyamapori hao.
Post A Comment: