WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameipongeza Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia kwa kazi kubwa ya kuratibu masuala ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu nchini huku akiumia nafasi hiyo kueleza Serikali ya Awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imedhamira kuendelea kuweka mikakati madhubuti katika eneo la sayansi, teknolojia na ubunifu.
Akisoma hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, kwenye Kongamano la Nane la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu lililofanyika jijini Dar es Salaam Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM) Profesa Lugano Kusiluka aliyemwakilisha mgeni rasmi amesema Tume imekuwa mstari wa mbele kusimamia mfumo wa sayansi, teknolojia na ubunifu.
Amesema mojawapo ya matunda yake ya Tume hiyo ni hilo kongamano la kitaifa na kwamba matarajio yake kwamba moja ya matokeo katika kongamano hilo, yatakuwa ni mapendekezo ya uboreshaji wa dira, sera, mipango na mikakati inayolenga kuboresha ukuaji na uendelezaji wa Sayansi,Teknolojia na Ubunifu kwa maendeleo endelevu.
"Napenda kuwahakikishia kwamba Wizara inatambua na juhudi zinazofanywa na watafiti, wanasayansi, wabunifu na wajasiriamali na itaendelea kuweka mazingira bora ili utafiti na ubunifu viweze kuwa na mchango mkubwa zaidi katika ukuaji wa uchumi.
"Natambua pia kuna wanasayansi Watanzania waliopo nje ya nchi, nipende kuwahakikishia Serikali, kupitia Wizara inaendele kuweka mazingira wezeshi ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuendeleza masuala ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu hapa nchini, " amesema.
Akifafanua zaidi Profesa Kusiluka amesema maendeleo ya kiuchumi na kijamii hayawezi kufikiwa bila kuwa na mipango madhubuti, ndiyo maana, kwa upande wa serikali, mojawapo ya hatua ilizozichukuliwa ilikuwa ni kuhakikisha shughuli za utafiti na maendeleo zinatengewa fedha zaidi ili kuendeleza ukuaji wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa maendeleo endelevu.
"Kama ilivyofanya katika ujenzi wa maabara na shule za sekondari za kata, kuanzisha programu maalum za mafunzo kwa walimu wa Hisabati na kutoa mikopo kwa asilimia 100 kwa wanafunzi wanaosoma mchepuo wa Sayansi katika sekondari;
"Kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaochukua masomo ya Sayansi na Teknolojia vyuo vikuu, kuongeza vyuo vya ufundi na maarifa, na kuhimiza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za jamii, katika kilimo na viwanda ili kuinua tija na utendaji kazi.
"Na kuendelea kuhimiza uanzishwaji wa kumbi za ubunifu katika ngazi za Halmashauri ili kuongeza chachu kwa vijana kuweza kubuni na kujipatia ajira. Serikali itaendeleza juhudi za kuboresha na kutekeleza sera ya Sayansi, Teknolojia kwa lengo la kukuza uelewa na kujenga utamaduni wa kutumia matokeo ya utafiti katika kuboresha sekta ya uzalishaji (kilimo na chakula, nishati, afya, viwanda, na uendelevu wa mazingira), " amesema.
Aidha, serikali itaendelea na utaratibu wa kugharimia shughuli za utafiti na ubunifu na kutoa fursa kwa Watanzania watakaopenda kujikita kielimu katika taaluma za sayansi na teknolojia.
Pia amesema amesikia kuwa baada ya Wiki ya Ubunifu iliyofanyika Mei 2023, kulikuwa na kikao mtandaoni na Watanzania wabobezi walioishi nje ya nje (Diaspora) ambapo COSTECH ilifanya wasilisho kuhusiana na wabunifu waliopo na mfumo wa ubunifu nchini kwa ujumla wake, na kwamba hawa watanzania wenzetu walipata fursa ya kushiriki online mkutano huu.
"Nafahamu kuwa Desemba 2022 Diaspora walifanya mkutano wao hapo COSTECH ambapo baadhi walikuja nchini na wengine walishiriki kwa njia ya mtandao. Nitumie nafasi hii kuwapongeza na kuwahakikishia kuwa Wizara itaendelea kutambua mchango wa wanasayansi Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) kuhusu masuala ya Sayansi na Teknolojia ili kubadilishana uzoefu katika nyanja mbalimbali.
"Kongamano hili ni sehemu pekee ambayo wadau wote wamepata fursa ya kukutana na kubadilishana uzoefu. Ni matarajio yangu kwamba baada ya kongamano hili kumezaliwa mashirikiano na mahusiano mapya au kuongeza nguvu ya yale yaliyopo kati ya watafiti, wabunifu, jamii za kimataifa na za kikanda, wenye viwanda, na serikali." amesema.
Pia katika kuongeza ushindani wa tafiti zenye tija hapa nchini, Serikali kupitia Wizara inahimiza wanasayansi na watafiti kuchapisha matokeo ya tafiti katika majarida nguli (high impact journals) ya kikanda na kimataifa.
Amefafanua Serikali imetenga shilingi za Kitanzania Bilioni moja kama tuzo kwa watafiti watakaoweza kuchapisha tafiti zao katika majarida hayo.Hivyo ni matumaini ya Wizara kwamba kama watatumia vizuri Sayansi, Teknolojia na ubunifu; wanaweza kuongeza tija na hivyo kupunguza gharama za upatikanaji wa huduma za afya, elimu, kilimo, nishati, mawasiliano, uchukuzi na sekta nyingine nyingi ikiwemo kuzalisha ajira kwa Watanzania wenzetu.
Pamoja na maelezo hayo amesema Ilani ya Chama Tawala Chama Cha Mapinduzi (2020 - 2025) na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26) vinasisitiza matumizi ya Sayansi, Teknolojia, na Ubunifu (STU) kama nyenzo muhimu ya kufikia maendeleo endelevu nchini ikijumuisha; ugunduzi wa mbegu na miche bora, matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na ujenzi wa uchumi imara na endelevu kwa nchi.
Katika kutekeleza maelekezo yaliyoko kwenye Ilani na Sera mbalimbali za kitaifa na kimataifa, Serikali iliunda Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili isaidie katika kuandaa Watanzania walioelimika na wenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa.
Post A Comment: