Zaidi ya Wananchi 40,000 wanaohudumiwa na kituo cha afya cha Ketumbeine kilichopo Wilayani Longido Mkoani Arusha wataanza kunufaika na msaada wa vifaa tiba vilivyotolewa na wadau wa maendeleo kwa lengo la kuwezesha huduma za upasuaji hususan kwa wanawake wajawazito wanaolazimika kujifungua kwa njia ya upasuaji.
Akikabidhi Msaada huo wa vifaa tiba Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NCBA Claver Serumaga amesema kuwa benki hiyo imejizatiti katika kusaidia jamii inayowazunguka na katika kipindi wameamua kutoa msaada huo katika katika kituo cha Afya cha Kitumbeine kinachohudumia Zaidi ya watu 40,000.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa wametoa vifaa vya kufanya upasuaji kusaidia huduma ya upasuaji katika kituo hicho cha Afya ambacho kitaanza kutoa huduma hizo hivi karibuni kwani watu wengi wanahitaji huduma hiyo.
“Msaada huu utasaidia kusogeza huduma za afya karibu na watu tumefurahi na tutaendelea kutoa misaada kwani huu ni mwanzo na tutaendelea kufanya kazi Pamoja”
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dr.Silvia Mamkwe akipokea msaada huo ameipongeza benki ya NCBA kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia jamii ya watu wa Longido ambao ni wafugaji ili waweze kujifungulia katika vituo vya afya kwani tayari serikali imeboresha huduma za afya na kupeleka wataalamu wa afya wa kutosha.
Naye Mganga Mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Longido Dr.Selemani Mtenjela amesema wamepokea kitanda maalumu kwa ajili ya kupima mgonjwa Pamoja na vifaa vya kufanya upasuaji ambavyo vitasaidia kuokoa Maisha ya Wajawazito ambao walikua wakitembea kilomita 60 kufuata huduma za upasuaji katika hospitali ya Wilaya.
Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Kitumbeine Dr.Frank Albert amesema kuwa kwa msaada walioupata watapunguza kutoa rufaa kwa wajawazito Kwenda hospitali ya wilaya kwani kwasasa wamejitosheleza kuanza kufanya upasuaji.
Post A Comment: