Na Imma Msumba ;Arusha
Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Anjela Kairuki amewataka wakurugenzi kutoka halmashauri zote nchini kutumia siku 30 zilizobaki kuhakikisha wanafikia malengo ya makusanyo waliojiwekea.
Amesema kuwa kwa wakurugenzi wote ambao hawatafikia malengo hasa yaliyosababishwa na uzembe watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Kairuki ameyasema hayo wakati akifunga mkutano mkuu wa 37 wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT), uliomalizika leo jijini Arusha katika ukumbi wa mikutano wa AICC.
"Naomba niwakumbushe wakurugenzi wote nchini kuwa tumebakiza mwezi mmoja tu kufunga mwaka wa fedha wa kiserikali na hadi ripoti ya April makusanyo yenu ni asilimia 77 tu, nawahimiza nendeni mkaongeze nguvu na kuimarisha makusanyo mfikie Lengo kabla hatua zijawafuata"
Waziri Kairuki alisema kuwa ziko baadhi ya halmashauri zimekuwa zinazotia mashaka katika makusanyo ya kwa kupuuzia baadhi ya vyanzo vya msingi vya mapato ikiwemo kushindwa kuidhinisha leseni za biashara kidigitali (mfumo wa Tausi), kuzima mashine za kukusanyia mapato (POS) na kubaki na fedha mkononi bila kuziingiza benki.
"Tutafikiaje malengo ya makusanyo Kama vitu vya msingi na vyanzo vyetu vikuu mnapuuzia? Sasa nendeni mkafanye ndio ajenda yenu na mkashirikiane na watendaji wenu hasa maafisa biashara, afya na mazingira kikubwa mfikie malengo"
Alisema kuwa kwa mujibu wa ripoti mbali mbali za mkaguzi mkuu wa Serikali, zimebaini kuwa zipo halmashauri zinatumia fedha kinyume na taratibu lakini pia zingine zinatumika bila kupitia kwenye mfumo rasmi wa kiserikali.
"Kwa hili nendeni mkajitathimini lakini pia jibuni hoja za CAG vema"
Kwa upande wake makamu mwenyekiti wa ALAT, Sima Constantine mbali na kumpongengeza Rais kwa kuwapatia fedha nyingi kwenye halmashauri za kutekeleza miradi yao, lakini pia wameahidi kwenye kuweka nguvu kwenye makusanyo kufikia malengo.
"Tunampongeza Rais Samia kwa kuona umuhimu wetu hasa katika kutupatia fedha nyingi za maendeleo na tunaahidi kwenda kuzisimamia vema na kutekeleza maagizo ya makamu wa Rais na Waziri wa TAMISEMI kwenye ukusajyaji mapato"
Zaidi walimuomba Rais Samia kuangalia upya namna ya kuboresha maslahi ya madiwani ikiwemo kuongezewa posho.
Awali mkuu wa wilaya ya Arusha Felisian Mtahengerwa alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wajumbe wote kutembelea hifadhi za Arusha ili kuwa mabalozi wazuri wa utalii nchini na kuongeza pato la Taifa.
Post A Comment: