Zoezi la Uelimishaji na uhamasishaji wa utoaji wa taarifa za madhara ya dawa ukifanyika Hospitali ya Kiomboi wilayani Iramba mkoani Singida.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Kati imefanya uelimishaji na uhamasishaji wa utoaji wa taarifa za madhara yanayohisiwa kusababishwa na dawa katika Halmashauri za Wilaya ya Iramba na Manyoni mkoani Singida.

Akizungumza wakati wa zoezi la uelimishaji lililofanyika kwa nyakati tofauti wiki hii, Mkaguzi wa Dawa kutoka TMDA, Seraphina Omolo alisema lengo kubwa ilikuwa ni kutoa uelimishaji na uhamasishaji wa utoaji wa taarifa za madhara yanayohisiwa kusababishwa na dawa,chanjo na vifaa tiba katika maeneo ya kutolea huduma za afya ikiwemo hospitali, vituo vya afya na zahanati.

‘”Zoezi hili liliwalenga watoa huduma za afya kuhusu utoaji wa  taarifa za madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi ya dawa, chanjo na vifaa tiba ili kuendelea kulinda afya ya jamii,” alisema Omolo.

Omolo alisema katika mafunzo hayo, watoa huduma hao walisisitizwa kutoa taarifa mara moja endapo watakutana na bidhaa duni za dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Aidha, Omolo alisema utoaji wa taarifa za madhara hayo pamoja na kutoa taarifa za bidhaa duni hurahisisha katika udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa dawa na hivyo jamii kulindwa kutokana na athari ambazo zingeweza kutokea.

Omolo alitaja moja ya jukumu kubwa  la TMDA kuwa ni kulinda afya ya jamii kwa kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Kwa upande wake Mkaguzi wa Dawa,  Octavian Ngoda alisema kutoa taarifa za madhara ni jukumu ambalo lipo kisheria ambapo  watoa huduma  wanapaswa kuzitoa hata kama ni maudhi madogo madogo ya kupata homa au kusikia kichefu chefu na sio yale madhara makubwa ambayo yanaweza kusababisha  mgonjwa kulazwa, kupata ulemavu au kufariki

Zoezi hilo likifanyika Kituo cha Afya cha Ndago wilayani Iramba.
Uelimishaji huo ukifanyika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni.
Ulimishaji huo ukiendelea,  Hospitali ya Kilimatinde wilayani Manyoni.
Uelimishaji ukiendelea.
 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: