Na Dotto Mwaibale, Manyoni
SHUJAA wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) Kata ya Manyoni mkoani Singida wametumia masaa manne kutoa elimu kwa wapiga debe ya namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili
na kushiriki shughuli za kijamii kwa kufanya usafi wa mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata
hiyo, Wallece Shechambo alisema wanaendelea kutoa elimu hiyo katika kila kona
ya kata hiyo kwa kuzungumza na makundi ya watu ya rika mbalimbali ambayo ni wanafunzi, vijana, wanawake, wasichana na wazee.
Alisema kazi ya utoaji wa elimu hiyo imeonesha kufanikiwa kutokana na
muitikio mkubwa wa wananchi na kuwa walitoa elimu hiyo kwa wapiga debe wa
Stendi ya Hiace za kwenda Itigi ambao wameahidi kuwa mabalozi wazuri wa kupinga
vitendo hivyo.
Alisema baada ya kutoa elimu hiyo wakiwa na Afisa Afya wa wilaya hiyo, Seif
Swedy walikwenda kufanya usafi katika
mzunguko wa magari 'Round about' unao kutanisha
magari ya kutoka Mjini Manyoni, Singida na Itigi ambapo walitumia nafasi
hiyo kutoa elimu hiyo kwa wananchi pamoja na Wajasiriamali wadogo wanaouza mafuta ya alizeti katika eneo hilo.
Afisa Afya wa wilaya hiyo, Seif Swedy alisema usafi wa mazingira mbali ya
kuweka mandhari zuri ya mji pia unasaidia kuondoa uwezekano wa kuibuka kwa
magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na kuhara yanayosababishwa na uchafu.
"Tuna wapongeza SMAUJATA kwa kujitoa katika shughuli za usafi
wa mazingira katika mji wetu wa Manyoni tunaomba na taasisi nyingine nazo ziige
mfano huo kwani kazi hii siyo ya Serikali pekee bali ni ya kila mmoja
wetu," alisema Swedy.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Mwembeni, Saluthary Naaly alisema
muitikio wa wananchi katika jambo hilo unaleta matumaini makubwa katika eneo
hilo na wilaya nzima ya Manyoni na kuwa kazi hiyo itakuwa ni endelevu na lengo
likiwa kuifanya kata hiyo kuwa ya mfano na kuigwa.
Alisema mafanikio wanayo yapata yanatokana na ushirikiano mzuri walionao
kati ya viongozi wa kitongoji cha Mwembeni, SMAUJATA, wananchi na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Kemirembe
Lwota ambaye amekuwa bega kwa bega nao hasa pale wanapokuwa wakihitaji ushauri wake.
Wakati huo huo SMAUJATA Manyoni walitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia
Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, Vituo vya
afya na Zahanati kwani ni maeneo yanayotumika katika kutoa msaada kwa wahanga
wa ukatili.
"Watoto wamekuwa wakienda shuleni na kutumia madarasa kupata elimu
badala ya kukaa nyumbani ambako wengi wao wamekuwa wakikumbwa na vitendo vya
ukatili na hospitali zimekuwa zikitumika kwa ajili ya kutoa matibabu kwa watoto
ambao wameathirika na ukatili kama kubakwa, kukeketwa na vingine vingi hakika
kwa kazi hii kubwa aliyoifanya Rais wetu tuna kila sababu ya kumpongeza,"
alisema Hossen Kheri Mwenyekiti wa SMAUJATA wa Kata hiyo.
Aidha, Mratibu wa SMAUJATA wa Kata hiyo, Zena Salum alisema timu yao nzima
ilifanikiwa kuondoa sintofahamu iliyotokea baina ya familia mbili zikituhumiana
kwa kumuhusisha mmoja watoto hao kumbaka binti wa familia nyingine ambapo timu hiyo ilimchukua mtoto huyo wa
kike aliyedaiwa kubakwa na kumpeleka Hospitali ya Wilaya hiyo na baada ya
kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu ilibainika hakubakwa na yupo salama.
"Baada ya kupata majibu hayo tuliwakutanisha wazazi wa familia hizo
ambapo walishikana mikono na kurejesha uhusiano uliokuwepo awali kabla ya
kuzushwa kwa tuhuma hizo," alisema Salum.
Timu ya Mashujaa wa SMAUJATA walioshiriki katika kazi hiyo kubwa iliyotukuka kutoka katika kata hiyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Wallece Shechambo, Mwenyekiti waSerikali ya Kitongoji cha Mwembeni, Saluthary Naaly, Mwenyekiti wa SMAUJATA , Hossen Kheri, Mratibu wa SMAUJATA wa Kata hiyo, Zena Salum, Mtunza fedha, Joyce Peter, Makamu Katibu Mkuu, Neema Masabuni, Mjumbe wa SMAUJATA, Vicent Boniphace na Mjumbe, Matilda Musa.
Post A Comment: