Mashujaa wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) Kata ya Manyoni wakishiriki kufanya usafi katika mzunguko wa magari (Round about) wilayani humo kazi iliyofanyika juzi ikiongozwa na Afisa Afya wa Wilaya hiyo, Seif Swedy.


Na Dotto Mwaibale, Manyoni

SHUJAA wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA) Kata ya Manyoni mkoani Singida wametumia masaa manne kutoa elimu kwa wapiga debe ya namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili na kushiriki shughuli za kijamii kwa kufanya usafi wa mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata hiyo, Wallece Shechambo alisema wanaendelea kutoa elimu hiyo katika kila kona ya kata hiyo kwa kuzungumza na makundi ya watu ya rika mbalimbali ambayo ni wanafunzi, vijana, wanawake, wasichana na wazee.

Alisema kazi ya utoaji wa elimu hiyo imeonesha kufanikiwa kutokana na muitikio mkubwa wa wananchi na kuwa walitoa elimu hiyo kwa wapiga debe wa Stendi ya Hiace za kwenda Itigi ambao wameahidi kuwa mabalozi wazuri wa kupinga vitendo hivyo.

Alisema baada ya kutoa elimu hiyo wakiwa na Afisa Afya wa wilaya hiyo, Seif Swedy walikwenda kufanya usafi katika mzunguko wa magari 'Round about' unao kutanisha magari ya kutoka Mjini Manyoni, Singida na Itigi ambapo walitumia nafasi hiyo kutoa elimu hiyo kwa wananchi pamoja na Wajasiriamali wadogo wanaouza mafuta ya alizeti katika eneo hilo.

Afisa Afya wa wilaya hiyo, Seif Swedy alisema usafi wa mazingira mbali ya kuweka mandhari zuri ya mji pia unasaidia kuondoa uwezekano wa kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na kuhara yanayosababishwa na uchafu.

"Tuna wapongeza SMAUJATA kwa kujitoa katika shughuli za usafi wa mazingira katika mji wetu wa Manyoni tunaomba na taasisi nyingine nazo ziige mfano huo kwani kazi hii siyo ya Serikali pekee bali ni ya kila mmoja wetu," alisema Swedy.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Mwembeni, Saluthary Naaly alisema muitikio wa wananchi katika jambo hilo unaleta matumaini makubwa katika eneo hilo na wilaya nzima ya Manyoni na kuwa kazi hiyo itakuwa ni endelevu na lengo likiwa kuifanya kata hiyo kuwa ya mfano na kuigwa.

Alisema mafanikio wanayo yapata yanatokana na ushirikiano mzuri walionao kati ya viongozi wa kitongoji cha Mwembeni, SMAUJATA, wananchi na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Kemirembe Lwota ambaye amekuwa bega kwa bega nao hasa pale wanapokuwa wakihitaji ushauri wake.

Wakati huo huo SMAUJATA Manyoni walitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, Vituo vya afya na Zahanati kwani ni maeneo yanayotumika katika kutoa msaada kwa wahanga wa ukatili.

"Watoto wamekuwa wakienda shuleni na kutumia madarasa kupata elimu badala ya kukaa nyumbani ambako wengi wao wamekuwa wakikumbwa na vitendo vya ukatili na hospitali zimekuwa zikitumika kwa ajili ya kutoa matibabu kwa watoto ambao wameathirika na ukatili kama kubakwa, kukeketwa na vingine vingi hakika kwa kazi hii kubwa aliyoifanya Rais wetu tuna kila sababu ya kumpongeza," alisema Hossen Kheri Mwenyekiti wa SMAUJATA wa Kata hiyo.

Aidha, Mratibu wa SMAUJATA wa Kata hiyo, Zena Salum alisema timu yao nzima ilifanikiwa kuondoa sintofahamu iliyotokea baina ya familia mbili zikituhumiana kwa kumuhusisha mmoja watoto hao kumbaka binti wa familia nyingine ambapo timu hiyo ilimchukua mtoto huyo wa kike aliyedaiwa kubakwa na kumpeleka Hospitali ya Wilaya hiyo na baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu ilibainika hakubakwa na yupo salama.

"Baada ya kupata majibu hayo tuliwakutanisha wazazi wa familia hizo ambapo walishikana mikono na kurejesha uhusiano uliokuwepo awali kabla ya kuzushwa kwa tuhuma hizo," alisema Salum.

Timu ya Mashujaa wa SMAUJATA walioshiriki katika kazi hiyo kubwa iliyotukuka kutoka katika kata hiyo wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Wallece Shechambo, Mwenyekiti waSerikali ya Kitongoji cha Mwembeni, Saluthary Naaly, Mwenyekiti wa SMAUJATA , Hossen Kheri, Mratibu wa SMAUJATA wa Kata hiyo, Zena Salum, Mtunza fedha, Joyce Peter, Makamu Katibu Mkuu, Neema Masabuni, Mjumbe wa SMAUJATA, Vicent Boniphace na Mjumbe, Matilda Musa.
Mashujaa wa SMAUJATA wakiendelea kupanga mikakati yao ya kazi. Kulia ni Mjumbe wa SMAUJATA wa kata hiyo, Mzee Juma Mahiki.
Share To:

Post A Comment: