Mashujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA)  Kata ya Manyoni mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja na Mzee Dominick Kijuu (mwenye kofia) aliyetoa eneo la ekari 4 kwa ajili ya kujenga shule eneo la Mtoo Kitongoji cha Mwembeni wilayani humo. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Serikali wa kitongoji hicho, Saluthary Naaly,Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata hiyo, Wallace Sichambo na Katibu wa Smaujata wa kata hiyo, Sarah Yohana.

Na Dotto Mwaibale, Manyoni

SHUJAA wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii (SMAUJATA)  Kata ya Manyoni mkoani Singida imeendelea kuwa moto wa kuotea mbali katika mapambano dhidi ya vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia ambapo ndani ya wiki moja wameweza kuwapata mashujaa wapya 50 ambao wataongeza nguvu ya mapambano hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Kata ya Manyoni, Wallace Shechambo alisema mashujaa hao wapya wamepatikana kupitia kampeni yao ya Wawili kwa Wawili ' Two by Two ambayo waliianzisha hivi karibuni na sasa inaonesha kupata mafanikio makubwa.

"Kampeni yetu ya 'Two by Two' imekuwa ya mafanikio na nina amini hadi kufikia mwezi Septemba tutakuwa na mashujaa wapya zaidi ya 150 ambao watatusaidia kuongeza nguvu ya mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili hasa kwa wanawake na watoto," alisema Shechambo.

Shechambo akizungumzia baadhi ya kazi walizozifanya mwezi huu wa Juni, 2023 alisema walifanya kazi za usafi wa mazingira katika kata hiyo kuzunguka viunga kadhaa vya mji wa Manyoni ikiwa ni pamoja na mzunguko wa magari 'Round About' ya kutoka Itigi na Singida.

Alisema baada ya kufanya usafi huo viongozi wa SMAUJATA walipata fursa ya kutoa elimu ya kuukataa ukatili kwa wananchi walioshiriki kufanya usafi huo zoezi lililoongozwa na Afisa Afya wa Wilaya hiyo Swedy Seif.

Shechambo katika mkutano huo alitoa elimu ya uzalendo na namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili katika kata hiyo na wilaya nzima ya Manyoni

Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Mwembeni Saluthary Naaly akizungumza katika mkutano huo alipata fursa ya kutoa elimu kuhusu ulinzi shirikishi ambao ni muhimu katika kukabiliana na vitendo vya ukatili.

"Bila ya kuwa na ulinzi shirikishi hatutaweza kukabiliana na vitendo vya ukatili niwaombe tuongeze nguvu katika jambo hili hakika tutafanikiwa," alisema Naaly.

Kwa upande wake Katibu Msaidizi wa SMAUJATA wa kata hiyo, Shujaa Neema Masabuni alitoa rai kwa walezi na wazazi kuwa makini wanapozungumza mbele ya watoto hasa mambo ya ndani yanayohusu mahusiano au kutoleana lugha za matusi wanapokuwa wamekoseana.

Mwenyekiti wa SMAUJATA wa kata hiyo Hussein Kheri alitoa shukurani kwa wananchi walioshiriki katika zoezi hilo ambalo lilikuwa na faida mbili ya kufanya usafi na kupata elimu yakupinga vitendo vya ukatili.

Mzee Mtundu ambaye ni mmoja wa mashujaa wa kata hiyo aliwashauri wazazi na walezi kujenga urafiki na watoto wao jambo litakalosaidia kujua changamoto walizonazo na kuwapatia msaada.

Mashujaa waliokuwa katika kampeni hiyo ni Afisa Afya wa Wilaya ya Manyoni, Swedy Seif, Saluthary Naaly, Hussein Kheri,  Joyce Peter, Neema Masabuni, Zena Salum, Mary Vicent, Juma Mpangala, Mary Dominick, Wallace Shechambo, Mwalimu Juma Mtundu.

Katika tukio jingine mashujaa wote wa kata hiyo wakiongozwa na viongozi wao walimpongeza Mzee Domonick Kijuu, Mzalendo wa ukweli ambaye ameunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha watoto wanapata mazingira mazuri ya kusomea ambaye ametoa eneo lake la ekari 4 bure kwa ajili ya ujenzi  wa Shule ya Msingi eneo la Mtoo katika Kitongoji cha Mwembeni.

Wananchi wa kata hiyo pamoja na viongozi wa SMAUJATA wakiongozwa na Mzee Kijuu (75)walikwenda kufanya usafi katika eneo hilo ambapo Mwenyekiti wa Serikali wa Kitongoji  cha Mwembeni Saluthary Naaly alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi umuhimu wa ujenzi wa shule katika eneo hilo kwani watoto wao wanao kadiriwa kuwa ni zaidi ya 450 hutembea umbali mrefu wa kwenda kupata elimu Shule ya Msingi Mwembeni na Manyoni huku wakipata adha kubwa wakati wa mvua za masika kwa barabara kujaa maji na kuhatarisha maisha yao kutokana na mafuriko.

Mzee Kijuu akizungumza wakati wakifanya usafi katika eneo hilo alisema amekuwa na furaha ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na Mkoa wa Singida kwa kutoa eneo hilo ambalo itajengwa shule kwa ajili ya kuwaandaa viongozi wa kesho.

"Nimelitoa eneo hili nililolitunza kwa muda mrefu nikiwa na akili timamu kwa ajili ya kujenga shule itakayo waondolea adha watoto kutembea umbali mrefu kwenda Shule ya Msingi Mwembeni na Manyoni kupata elimu," alisema Mzee Kijuu.

Wakizungumza katika eneo hilo wananchi waliofika kufanya usafi wakiwa na wanafunzi wa darasa la tatu na sita wanaoishi nao, walimshukuru mzee huyo kwa kutoa eneo na kupendekeza shule hiyo ikijengwa iitwe Shule ya Msingi Kijuu ili kumuenzi.

Aidha, katika tukio lingine mashujaa wa kata hiyo ya Manyoni walikwenda kwenye Kitongoji cha Tambukareli ambako walikuwa wamealikwa kwenye mkutano wa hadhara na Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Aziza Mbago kwa ajili ya kutoa elimu ya kupinga ukatili na kuzungumzia kampeni yao ya 'Two by Two'.

Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Kata ya Manyoni akizungumza katika mkutano huo aliwataka wananchi kuwa wazalendo na kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili ambavyo vimekithiri miongoni mwa jamii na kueleza kuwa moja ya njia ya kuvipunguza wazazi kuheshimiana, kuthaminiana na kunawajenga watoto kwa kuamini kuwa nyumbani kwao ni sehemu sahihi ya kuishi badala ya kuwaacha wakitangatanga mitaani.

Shujaa Henry Mallya akizungumzia wazazi waliotengana alisema ni muhimu kujua mazingira alipo mzazi mwenzie ili waweze kusaidia katika malezi ya watoto au hata kumpata  pale mmoja kati yao atakaposhindwa kutimiza wajibu wake wa matunzo kwa familia husika jambo litakalo punguza kuwepo kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Kwa upande wake Katibu wa SMAUJATA Kata ya Manyoni, Sarah Yohana alizungumzia wajibu wa  wazazi wote wawili katika malezi ya watoto wao.

Mwenyekiti wa Kitongoji hicho cha Tambukareli Shujaa Aziza Mbogo alisema kampeni ya 'Two by Two' ndio mkombozi katika kutokomeza ukatili katika wilaya hiyo.

Mashujaa wa SMAUJATA waliohudhuria mkutano huo katika Kitongoji hicho cha Tambukareli uliokuwa na wananchi zaidi ya 100 ni Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Kata ya Manyoni, Wallace Shechambo, Katibu, Sarah Yohana, Mtunza Hazina, Joyce Peter  Mratibu wa SMAUJATA, Zena Salumu, Mshauri wa SMAUJATA, Henry Mallya na Matilda

Katibu wa SMAUJATA Kata ya Manyoni, Sarah Yohana, akitoa elimu katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kitongoji cha Tambukareli.
Mwenyekiti wa Serikali wa Kitongoji cha Mwembeni, Saluthary Naaly, akitoa elimu ya kupinga ukatili kwa kushirikisha ulinzi shirikishi wakati wa mkutano uliofanyika Kitongoji cha Tambukareli. 
Elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia ikifanyika baada ya zoezi la kufanya usafi lililoongozwa na Afisa Afya wa Wilaya ya Manyoni, Swedy Seif.
Elimu hiyo ikitolewa.
Watoto wa darasa la tatu na sita wanaoishi katika kitongoji hicho walio shiriki kufanya usafi wa eneo la kiwanja hicho.
Mkutano wa hadhara Kitongoji cha Tambukareli ukifanyika.
Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA wa Kata ya Manyoni, Wallace Shechambo akitoa elimu ya upingaji wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Mkutano wa hadhara ukifanyika.
 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: