Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Mkakati Mpya wa Shirika la WATERAID Tanzania (2023-2028) na Maadhimisho ya WATERAID nchini kwenye ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameielekeza Wizara ya Maji iendelee kushirikiana na wadau wa sekta ya maji kukamilisha miradi yote inayoendelea kutekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Pia, Waziri Mkuu amesema Wizara ya Maji itengeneze na kutekeleza mwongozo wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ili kuimarisha uwekezaji katika sekta ya maji kwa kushirikiana na wadau wote muhimu.
Ametoa maelekezo hayo leo (Jumanne, Juni 13, 2023) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye uzinduzi wa Mpango wa Nchi wa WaterAid (2023-2028) na maadhimisho ya miaka 40 ya Shirika la WaterAid Tanzania. Hafla hiyo imefanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua mchango wa Shirika la WaterAid katika kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa awamu zote za utekelezaji wake.
“Na leo kupitia maadhimisho haya, sina budi kuwapongeza Shirika la WaterAid Tanzania kwa kutimiza miaka 40 ya kazi nzuri mnayofanya ya kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi ambayo imeweza kuleta mafanikio makubwa.”
Pia, Waziri Mkuu amewashukuru wadau wa waendeleo kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali nchini, na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao na itazingatia makubaliano, miongozo na taratibu zote ili kuhakikisha kwamba wanatekeleza miradi mingi zaidi mijini na vijijini kwa maslahi ya Watanzania.
Kadhalika, Waziri Mkuu amezitaka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI zitenge fedha za kutosha kuwezesha utekelezaji wa Mwongozo wa Mpango Kabambe wa Afya wa Halmashauri (CCHP). “Hii itasaidia kupatikana kwa huduma muhimu za maji safi na salama, vyoo bora na vifaa vya kunawia mikono zinatekelezwa kwenye vituo vyote vya elimu na afya hapa nchini.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Mary-Prisca Mahundi amesema makisio ya bajeti ya Mpango wa Nchi wa WaterAid (2023-2028) ni shilingi bilioni 45.87 ambapo kuna ongezeko la shilingi bilioni 9.07 ikilinganishwa na mpango uliopita.
Amesema fedha zilizotengwa kwenye mpango mpya zitatumika kuboresha sekta ya maji katika maeneo ya huduma endelevu, jumuishi na salama ili kuleta mabadiliko makubwa. “Nitumie fursa hii kuwapongeza WaterAid Tanzania kwa kutekeleza mpango wao uliopita.”
Pia, Naibu Waziri amewashukuru wadau wote wa maendeleo wanaochangia katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya sekta ya maji kwa kuwa michango yao ya kifedha na kitaaluma ni muhimu katika kuendeleza na kuboresha utoaji huduma.
Awali, Mkurugenzi Mkaazi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga alisema shirika hilo katika kipindi cha miaka 40 tangu lianze kazi nchini, limeweza kushirikiana na Serikali kuwafikishia huduma za maji watu milioni nane, ambapo watu 800,000 walipatiwa vyoo bora na watu milioni 26 walihamasishwa masuala ya usafi wa mazingira wanayofanyia kazi katika mikoa 11 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema katika utekelezaji wa kampeni ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani, WaterAid kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo watahakikisha kampeni hiyo inafanikiwa na maji yanapatikana.
Akizungumzia kuhusu mkakati mpya wa WaterAid uliozinduliwa leo, Bi Mzinga alisema utazingatia maeneo makuu mawili ambayo ni kufikia huduma endelevu, jumuishi na salama za maji, vyoo na usafi binafsi kwenye maeneo lengwa ya kijiografia pamoja na kutoa kipaumbele cha maji, vyoo bora na usafi binafsi katika sekta ya afya ili kuboresha afya ya umma.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata keki ya Maadhimisho ya miaka 40 ya Shirika la WATERAID nchini kwenye ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam, Juni 13, 2023. Wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, Mkurugenzi Mkaazi wa WATERAID nchini, Anna Tenga Mzinga na Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini a Zanzibar, Shaibu Hassan Kadura.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionesha nakala ya Mpango Mpya wa Shirika la WATERAID nchini (2023-2028) baada ya kuzindua mpango huo kwenye ukumbi wa hoteli ya Serena jijini Dar es salaam, Juni 13, 2023. Wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, Mkurugenzi Mkaazi wa WATERAID nchini, Anna Tenga Mzinga na kulia ni Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar, Shaibu Hassan Kadura
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea tuzo kutoka kwa Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la WATERAID, Anna Tenga Mzinga, ya Miaka 40 ya Shirika la WATERAID ya kutambua mchango wake katika kufanikisha majukumu mbalimbali ya shirika hilo, katika Maadhimisho ya miaka 40 ya Shirika la WATERAID nchini Tanzania kwenye ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam, Juni 13, 2023.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mkakati Mpya wa Shirika la WATERAID Tanzania (2023-2028) na Maadhimisho ya WATERAID nchini kwenye ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam, Juni 13, 2023.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mkakati Mpya wa Shirika la WATERAID Tanzania (2023-2028) na Maadhimisho ya WATERAID nchini kwenye ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam, Juni 13, 2023.
Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la WATERAID, Anna Tenga Mzinga, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mkakati Mpya wa Shirika la WATERAID Tanzania (2023-2028) na Maadhimisho ya WATERAID nchini kwenye ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar es salaam, Juni 13, 2023.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye hoteli ya Serena jijini Dar es salaam kuzindua Mkakati Mpya wa Shirika la WATERAID Tanzania (2023-2028) na Maadhimisho ya WATERAID nchini , Juni 13, 2023.
Post A Comment: