Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akifungua bomba la maji kuashiria uzinduzi wa mradi wa maji wa Kijiji cha Iglansoni katika hafla iliyofanyika Juni 5, 2023 wilayani Ikungi. Kulia ni Mkuu wa wilaya hiyo, Thomas Apson.
Na Dotto Mwaibale, Ikungi
MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba amewaagiza maafisa manunuzi katika halmashauri za wilaya
mkoani hapa kuweka mafundi wengi kwenye miradi inayotekelezwa kwa 'force
acount' badala ya kutoa zabuni kwa mkandarasi mmoja ambao imebainika
wanachelewesha kuikamilisha.
Serukamba alitoa agizo hilo Juni 5, 2023 alipokuwa Wilaya ya Ikungi katika mfululizo wa ziara ya kutembelea na kukagua
miradi ya maendeleo na kuhimiza kukamilika
kabla ya mwisho wa mwezi huu.
"Niwaombe maafisa manunuzi muache kutoa zabuni za ujenzi wa miradi kwa
mkandarasi mmoja pale mradi husika
unapofanywa kwa njia ya force acount kwani tunaongeza gharama pasipo sababu
yoyote na wengi wa wakandarasi hao
wakekuwa wakichelewesha ukamilikaji wake kutokana na kuwa na kazi nyingi,"
alisema Serukamba.
Alisema utekelezaji wa miradi kwa njia ya 'force acount' baada ya kuunda
zile kamati tatu wanaitwa mafundi zaidi ya 10 na kushindanishwa kwa bei
kulingana na ujenzi unaofanyika na yule atakayeonekana kuwa na bei ya chini
ndio anayepewa kazi ya papo kwa papo kama kupiga ripu na kazi ya msimamizi wa
mradi huo ni kuandika taarifa ya kazi iliyofanyika na gharama yake.
Alisema inapohitajika kujenga ukuta au kupaua mafundi hao wanaitwa tena na
kushindanishwa na yule atakaye kuwa na
bei nzuri atapewa kazi hiyo na kuwa utaratibu huo utakuwa ukiendelea hadi
ujenzi utakapo kamilika na kuwa wakati huo vifaa vyote vinakuwa vimenunuliwa.
" Hii habari ya kumtafuta fundi mmoja mkubwa apewe kazi yote yeye na
kulipwa fedha zote alafu aanze kutafuta mafundi mara nyingi kazi hiyo inakuwa
haikamiliki kwa wakati na haraka
kutokana na kuwa na kazi nyingi," alisema Serukamba.
Alisema ukamilishaji wa miradi kwa njia ya force acount ni miradi kufanyika
kwa haraka na kupunguza gharama ya ujenzi na faida nyingine watakuwepo wananchi
ambao watajitolea na kuwa kazi kubwa ya madiwani ni kuwahamasisha wananchi
kujitokeza kujitolea.
Aidha, Serukamba aliwaomba wahandisi kwenda kutembelea na kukagua
inapotekelezwa miradi hiyo kwani uzoefu unaonesha huwa hawaendi inapofanywa kwa
njia ya 'force acount' wakiamini kazi hiyo haiwahusu bali inafanywa na kamati
zilizoundwa.
Serukamba alisema Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kutoa
fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo ambapo aliomba ikamilishwe kwa
viwango vinavyotakiwa na kwa thamani halisi na si vinginevyo.
Katika hatua nyingine Serukamba alizindua miradi ya maji miwili ya Kijiji
cha Iglansoni na Ihanja ambayo imetekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa
Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Ikungi ambayo inakwenda kuondoa
changamoto ya muda mrefu waliokuwa wakiipata wananchi wa maeneo ilipo miradi
hiyo ya kukosa maji.
Serukamba alitumia nafasi hiyo kuipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na
Mbunge wa Jimbo la Singida, Magharibi Elibariki Kingu kwa utekelezaji mzuri wa
miradi yote aliyoitembelea na akawahimiza kuhakikisha wanaongeza kasi ya
kuikamilisha kabla ya Juni 20,2023 ili ianze kufanya kazi ifikapo Julai 1,
mwaka huu.
Miradi aliyoitembelea na kuridhishwa nayo ni mradi wa maji katika Kijiji
cha Ihanja ambao pia utatoa huduma katika Kijiji cha Iseke, mradi wa maji wa
Kijiji cha Iglansoni, ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Malolo iliyopo
Kijiji cha Iglansoni, ujenzi wa barabara za Ihanja, Nduru, Nduru Makilawa na
Ikhakhamo- Mayaha-Ighombwe na ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari ya
Puma.
Mradi mwingine alioukagua ni ujenzi wa Kituo cha Afya Iglansoni ambao ujenzi wake umekamilika kwa sehemu kubwa na kuwa tayari Serikali imekwisha peleka baadhi ya vifaa tiba ambapo aliagiza hadi ifikapo Julai 1, 2023 kituo hicho kianze kutoa huduma za afya kwani hakuna sababu itakayo sababisha kisianze kufanya kazi.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Ikungi, Mhandisi Hopeness Liundi (mwenye miwani) akimuelekeza jambo Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba wakati akizindua rasmi mradi wa maji wa Kijiji cha Iglansoni.
Post A Comment: