Wananchi wanaoishi karibu na maeneo yenye migodi katika mkoa wa Shinyanga, wameanza kunufaika na uwepo wa shughuli za uchimbaji wa madini katika maeneo yao, kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inawezeshwa na makampuni ya uchimbaji wa madini.
Hayo yamebainishwa na Afisa Madini Mkazi wa mkoa wa Shinyanga Bw. Daniel Mapunda, wakati akizungumza kupitia kipindi maalum cha kuelimisha umma kuhusu namna ambavyo wananchi wananufaika na uwepo wa madini katika maeneo yao, kilichoandaliwa na Redio Faraja kwa kushirikiana na shirika lisilokuwa la kiserikali la HAKIRASLIMALI, ambalo linajihusisha na masuala ya utetezi wa kimkakati wa shughuli za uchimbaji wa madini, mafuta na Gesi.
Bwana Mapunda amebainisha kuwa, hatua hiyo imefikiwa baada ya marekebisho ya sheria ya madini yaliyofanyika mwaka 2017, ambayo iliweka kanuni maalum ya ushirikishwaji wa wazawa katika shughuli za uchimbaji wa madini (Local content) ili kuboresha faida za kiuchumi na kijamii zinazobaki ndani ya nchi, ambapo pamoja na mambo mengine, inamtaka mwekezaji mwenye leseni ya kuchimba madini kuwezesha shughuli za maendeleo kwa jamii inayomzunguka, kupitia mpango wa uwajibikaji kwa jamii unaojulikana kama Corparate Social Responsibility (CSR) pamoja na kuweka msisitizo katika ulipaji wa ushuru wa huduma kwa kiasi cha asilimia 0.3 ili kuchangia mapato ya ndani ya Halmashauri.
Sheria hiyo pia inaelekeza makampuni ya uchimbaji wa madini kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa na hasa zisizo na masharti ya kitaaluma, pamoja na kuhakikisha huduma zote zinazotolewa kwenye migodi zikiwemo za usafi, ulinzi, chakula na kandarasi mbalimbali zifanafanywa na wazawa, isipokuwa tu kwa zile zinazohitaji watu wa nje.
Bw. Mapunda amebainisha kuwa, Serikali kupitia vyombo vyake ikiwemo ofisi ya Kamishna wa madini, Benki kuu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na vyombo vya ulinzi na usalama inafuatilia kwa kina ili kudhibiti udanganyifu, hatua ambayo imekuwa na mafanikio makubwa na kuwafanya wawekezaji wengi na hasa wa migodi mikubwa kuwajibika kikamilifu katika kuwezesha shughuli za maendeleo kwenye jamii inayowazunguka, jambo ambalo limeimarisha mahusiano na kupunguza migogoro iliyokuwa ikitokea kipindi cha nyuma kati ya wawekezaji na wananchi.
Mapunda ameutolea mfano mgodi wa Almasi wa Williamson Diamonds LTD uliopo Mwadui wilayani Kishapu na kubainisha kuwa, mgodi huo unatekeleza sheria hiyo kwa kiwango cha kuridhisha, ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023, wameingia makubaliano ya CSR na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ya kuchangia kiasi cha Shilingi Bilioni 1.2, kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo katika vijiji 12, vinavyouzunguka mgodi huo.
Amekitaja kiasi hicho cha fedha kuwa ni kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo mgodi huo ulikuwa ukichangia kiasi kisichozidi Milioni 156 kwa mwaka.
Mapunda pia amekitaja kikundi cha wachimbaji wadogo cha WACHAPAKAZI kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga (Vijijini) kuwa, licha ya kuchangia mapato ya Serikali kwa kiasi cha Shilingi Bilioni 1.8, baada ya kufanyiwa ukaguzi wa mauzo yake ya mwaka mzima, pia kimewezesha miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo ya jirani ikiwemo kujenga vyumba vya madarasa na nyumba za Walimu na kwamba, ofisi yake inaendelelea kufuatilia ili kuhakikisha wachimbaji wote wenye leseni hasa wadogo na wa kati wanatekeleza sheria hiyo, inayotaka wananchi wanaozunguka maeneo ya uchimbaji kunufaika na uwepo wa madini katika maeneo yao.
Nao baadhi ya wakazi wa vijiji vinavyozunguka mgodi wa Mwadui, wamekiri kuanza kuona faida za uwepo wa mgodi huo katika eneo lao kutokana miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa kupitia CSR, ambayo ni pamoja na maboresho ya barabara, upanuzi wa miradi ya maji, ujenzi wa vituo vya Afya, ujenzi wa ofisi za kata na vijiji, ununuzi wa madawati, ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika shule za msingi na Sekondari.
Hata hivyo, miongoni mwa Wananchi hao wameonyesha kutoridhishwa na kiwango kinachotolewa na mgodi wa Mwadui ikilinganishwa na uwezo wake wa kuzalisha, ambapo wameomba ujitoe zaidi ili kuwezesha miradi mingi ya maendeleo, kwa kuwa bado maeneo mengi yanayozunguka mgodi huo yana uhitaji mkubwa kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukame, uhaba wa maji, umbali wa huduma za afya, ukosefu wa mabwawa kunyweshea mifugo, na baadhi ya vijiji kutokuwa na nishati ya umeme.
Pia wametumia nafasi hiyo kuuomba uongozi wa mgodi kupanua wigo wa fursa kwa wazawa, ikiwemo kuongeza nafasi za ajira hasa zile ambazo hazihitaji utalaam.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Afisa biashara wa Halmashauri hiyo Peter Wilbard, amesema kupitia fedha za CSR kiasi cha asilimia 0.7, za mauzo ya Almasi zinazotolewa na mgodi wa Mwadui kwa sasa, Halmashauri imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa kituo cha Mabasi cha Maganzo, ambapo kiasi cha asilimia 0.3 ya wanazozipata kupitia ushuru wa huduma (Service Leavy) wamekuwa wakizirejesha kwa wananchi kupitia miradi mbalimbali ya maenedeleo inayotekelezwa katika maeneo yote ya Halmashauri, ambayo ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa na maboresho ya shule, ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, kuboresho barabara, kusogeza huduma za maji na huduma nyingine za kijamii na kwamba, mgodi huo unaongoza kwa kuchagia kiasi kikubwa cha mapato ya ndani yanayotokana na ushuru wa huduma .
Kwa mujibu wa Meneja Mahusiano wa mgodi wa Mwadui Bw. Bernard Mihayo, mgodi huo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, umeweka mikakati mbalimbali ya kuendelea kupanua wigo wa kuwezesha huduma za kijamii kutegemeana na hali ya uzalishaji, ambapo kwa sasa uko kwenye mchakato wa kuanzisha mradi wa kilimo cha umwagiliaji ili kuwasaidia wananchi kukabiliana na hali ya ukame, na unaendelea kutekeleza mradi mwingine wa kutokomeza mfumo dume unaochangia vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.
Kulingana na taarifa ya ofisi ya Madini, mpaka sasa mkoa wa Shinyanga kwa upande wa wilaya mbili za Kishapu na Shinyanga pekee una jumla wachimbaji wadogo wenye leseni wapatao 200 na migodi mitano ya wachimbaji wa kati.
Post A Comment: