Na Kassim Nyaki, Dodoma


Waziri wa Malisili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa leo tarehe 2 Juni, 2023 akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo Bungeni jijini Dodoma amewapongeza Wananchi wanaoishi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuendelea kujiandikisha kwa hiari na kupisha shughuli za uhifadhi katika hifadhi hiyo.

Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa “Kuhusu zoezi la kuwahamisha wananchi kwa hiari kutoka eneo la Urithi wa Dunia la Ngorongoro, nawapongeza wananchi wote ambao kwa hiari yao walishajiandikisha na wanaendelea kujiandikisha kuhama kwa hiari kuhamia eneo la Msomera na maeneo mengine Nchini.

Amebainisha kuwa maeneo wananchi hao wanapohamia na kuendelea na maisha yao ni salama na wamepewa nyumba na maeneo ya kulisha mifugo yao na kupatiwa haki zao nyingine kama shule na kuwekewa mazingira wezeshi ya kufanya biashara, tofauti na walivyokuwa wakiishi kwa mashaka”

“Niwaahidi wananchi waliosalia na ambao wamekuwa wakijiandikisha kwa wingi na kwa shauku kutaka kuhama kuwa, zoezi hili bado halijasimamishwa na Serikali, tofauti na inavyosemekana kwa baadhi ya wanaojaribu kukwamisha” amefafanua Mhe. Mchengerwa

Mhe. Waziri ameliahidi Bunge kuwa, Serikali imejiandaa na ina rasilimali za kutosha za kukamilisha zoezi hilo na haitarudi nyuma wala hakutakuwa na kusalimu amri katika kukamilisha zoezi hili ambalo litaendelea kufanyika kwa weledi na kasi kubwa.

Akizungumzia kuhusu Uongozi wa Wizara hiyo na taasisi zake kukutana na kufanya vikao na wadau wa Uhifadhi na utalii Mhe Mchengerwa ameeleza kuwa

‘Kati ya Mei 25 hadi Juni 1 mwaka 2023, Wizara ilikutana na wadau wa kisekta wakiwemo wa wanyamapori, misitu, nyuki na utalii kwa lengo la kupitia changamoto na kuweka mikakati ya pamoja ya kutatua changamoto zilizopo katika sekta hizo.

Amewaahidi wadau hao kuwa Wizara itaendelea kuwa nao karibu, itawalinda, itatetea maslahi yao na zaidi nao watimize wajibu wao kwa Taifa kwa kulipa kodi na kufanya biashara zao kwa njia za halali”
Share To:

Post A Comment: