NAIBU Waziri wa MAJI, Mhandisi Maryprisca Mahundi ametoa msaada wa Shilingi Milioni 5,000,000 kwa Umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Mbeya Mjini kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Umoja huo pamoja kitegacuchumi.

Mahundi ambaye ni Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa Mbeya, alitoa msaada huo juzi aliposhiriki baraza la UWT la wilaya hiyo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake ya kutoa Sh. Milioni 5 kwa kila wilaya katika mkoa huo.

Akizungumza wakati akikabidhi fedha hizo, Mahundi aliupongeza umoja huo kwa kuanzisha mradi wa nyumba za kupangisha ambao alisema ukikamilika utakuwa ni miongoni mwa vyanzo vya mapato vya uhakika.

Alisema kabla ya kwenda kwenye baraza hilo alitembelea kwanza mradi huo na kubaini kwamba mradi unaendelea vizuri na hivyo akaona ni vizuri kuwashika mkono ili kasi iongezeke.

Alisema baada ya kutoa fedha hizo UWT Mbeya Mjini watakuwa wanamdai Sh. Milioni 13 ambazo aliahidi kuwa atazikamilisha hivi karibuni.

“Nawapongeza sana kwa mradi huu, sikuwa na lengo la kuwapa fedha zote hizi lakini baada ya kutembelea nimeridhika na nikawaambia wasaidizi wangu kwamba nachukua fedha kwenye fungu linguine ili zifike hizi nilizowapatia,” alisema Mahundi.

Aliwataka wadau mbalimbali kuendelea kuusaidia umoja huo ili ukamilishe mradi huo mapema na uanze kufanya kazi ya uzalishaji na kuufanya kuwa miongoni mwa vyanzo vya mapato vitakavyoufanya kujitegemea.

Aliutaka umoja huo pia kuendelea kuwaombea viongozi mbalimbali wa serikali ili watekeleze majukumu yao vizuri na kulifanya taifa kuwa na amani na utulivu.

Katibu wa UWT Wilaya ya Mbeya Mjini, Ruth Mwambusi alisema kwa sasa umoja huo hauna mradi wowote unaoingiza mapato lakini kwa sasa wameandaa mpango kazi wa kuhakikisha wanakuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato.

Alisema katika eneo ambalo wanajenga nyumba za kupangisha lilikuwa ni ghala ambalo lilikuwa halitumiki na hivyo kwa muda mrefu lilikuwa haliwaingizii mapato yoyote.

Alisema waliamua kubadili matumizi na kuamua kujenga nyumba za kupangisha ambazo zitakuwa na vyumba 11 na kwamba malengo yao ni kupangisha kwa Sh. 50,000 chumba kwa mwezi.

Alisema mbali na kujenga nyumba hizo za kupangisha pia wanaendelea na ujenzi wa nyumba ya kuishi ya Katibu wa UWT wa wilaya ili waondokane na adha ya kuishi kwenye nyumba ya kupanga.

“Tuliunda Kamati ya manunuzi ambayo ndiyo inayoshughulikia ujenzi wa mradi huu kwa kuhakikisha mradi unakwenda kwa kasi, tunashukuru kwamba tunashikwa mkono na wadau mbalimbali,” alisema Ruth.

Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mbeya, Edna Mwaigomole alimshukuru Naibu Waziri Mahundi kwa kuendelea kuisaidia jumuiya hiyo kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema umoja huo utaendelea kumuunga mkono kwenye shughuli mbalimbali anazofanya zikiwemo za ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya maendeleo.



Share To:

Post A Comment: