Tarehe 30 ya mwezi wa sita kila mwaka Jumuiya ya watu wa Kongo wanaoishi hapa nchini Tanzania hufanya tamasha maalumu la muziki wa dansi ikiwa ni sehemu ya kuhadhimisha uhuru wa nchi yao kiburudani zaidi, kwani wengi wao ni wanamuziki na wamekaa hapa nchini Tanzania kwa muda mrefu takribani miaka 20.Kwa mwaka huu wa 2023 kama ilivyo kawaida tamasha la burudani limeandaliwa na idadi ya bendi pamoja na wanamuziki wa dansi watakao tumbuiza tayari imewekwa bayana na hapo ndipo mjadala mkubwa ulipoanzia kwanini bendi nyingi pamoja na wanamuziki binafsi wasiokuwa na bendi walioalikwa wote ni kutoka jijini Dar es salaam na hakuna bendi yeyote wala mwanamuziki kutoka mikoani.
Kutokana na sintofahamu hii ndipo mwenyekiti wa chama cha muziki wa dansi hapa nchini Tanzania CHAMUDATA Bi Luizer Mbutu amezungumzia jambo hilo na kusema kuwa tamasha hilo la muziki halijahusisha CHAMUDATA kwenye uandaaji bali ni mtu binafsi ameandaa na ndio yeye aliyeamua aalike bendi gani kwenye tamasha hilo, hivyo wanamuziki na bendi za mikoani wasiilaumu CHAMUDATA ila kama ni mapendekezo na maboresho ya uandaaji yatafikishwa kwa muhusika kwa matamasha yajayo.
Pia Bi Luizer amesisitiza kuwa huenda wadau wengi wanakosa fursa mbalimbali kwasababu wengi wao bado hawajajiunga na chama hicho cha muziki wa dansi, hivyo ametoa wito kwa wanamuzki wote wa dansi kujisajili kwenye chama na njia ni rahisi kabisa, mwanamuziki yeyote amtafute kwa namba zake ili aweze kupatiwa fomu ya kujisajili na pesa ya fomu ni kiasi cha shilingi 10,000 na ada ya uanachama ni kiasi cha shilingi 12,000 kwa mwaka.
Kwa mwaka huu bendi zilizoalikwa ni Akudo impact chini ya Christian Bella , Fm Academia chini ya Nyoshi Elsadat, Diamond Musica chini ya Liva Hassan Sultan, Hamza Kalala na Nguza Viking, Tukuyu sound chini ya Kalala junior na Papii Kocha, Town Classic band, Twanga pepeta, Muuminin Mwinjuma na Jimmy Manzaka.
Tanzania ni moja kati ya nchi zenye wageni wengi sana ikiwemo raia wa Kongo wanaofika nchini kwa shughuli mbalimbali na wengi wao wakikaa Tanzania huwa hawatamani kuondoka kutokana na Amani na utulivu uliopo hapa nchini na baadhi yao walikuja na familia zao kama wakimbizi na hiyo imedhihirisha wazi Tanzania ni nchi ya Amani na kila mtanzania anapaswa kuilinda amani tuliyonayo kwa kungalia namna nchi zingine za Africa ikiwemo Kongo machafuko yalivyotanda kila kukicha. Amani yetu ndio fahari yetu.
Post A Comment: