Wafamasia wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila wametoa elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa katika Shule ya msingi na Sekondari Mloganzila ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya Famasi Tanzania.
Akiwasilisha mada kwa wanafunzi hao Mfamasia wa MNH-Mloganzila Bw. Kenneth Kiboganya amesema dawa kwa binadamu inatumika kwa mambo mawili ambapo ni kutibu maradhi na kumkinga mtu asipate maradhi na itafanya kazi vizuri endapo utatumia ipasavyo.
“Dawa inakazi muhimu sana kwa binadamu na endapo itatumika vibaya inaweza kuleta madhara makubwa kwa mtumiaji na wakati mwingine inaweza p kifo , hivyo hatupaswi kutumia dawa bila kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ”amesema Bw.Kenneth
Kwa upande wake Bw. Ammar Khamis ambaye pia ni Mfamasia wa Mloganzila ameongeza kuwa matumizi holela ya dawa yanaweza kupelekea mtu kupata usugu wa dawa hivyo ni vyema Kama mtu anahisi anaumwa afike kituo cha afya kwa ajili ya kufanya vipimo kwakuwa kila ugonjwa unamatibabu yake.
“Kabla ya kununua dawa unapaswa kwanza kwenda kwa daktari akuandikie dawa zitakazotibu tatizo lako, na ukienda kwa mfamasia kuchukua dawa unapaswa kuwa makini na kusikiliza maelekezo ya sahihi ya kutumia dawa hizo, endepo ukitumia kinyume na maelekezo ya wafamasia unaweza kusababisha baadhi ya viungo mwilini kushindwa kufanya kazi yake vizuri” amesema w. Khamis
Wiki ya Famasi Tanzania huadhimishwa kila tarehe 10 hadi 16, Juni kila mwaka ambapo wanafunzi zaidi 200 wa Shule ya Msingi na Sekondari wamepatiwa elimu hiyo.
Post A Comment: