]Wananchi wanaoishi kandokando ya Msitu wa Mafunzo wa Olmotonyi Mkoani Arusha wamekishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuwapatia nafasi ya kupata kuni pamoja na maeneo ya Kilimo na hivyo kusaidia kupata kipato cha kuendesha maisha yao na familia zao kwa miaka mingi.
Shukrani hizo zimetolewa na Wananchi hao wakati wakiongea na Waandishi wa habari ndani ya msitu huo unaomilikiwa na SUA ambao ni maalumu kwaajili ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaosoma
shahada mbalimbali za misitu katika Chuo hicho.
Akizungumza wakati akikata kuni kwenye eneo ambalo linavunwa Mbao kwa sasa Bi. Mami Lowasa amesema toka azaliwe amekuta wazazi wake wakiingia kwenye msitu huo wa Olmotonyi kukata kuni na hasa kulima kwenye maeneo ambayo uongozi wa Kituo hicho umekuwa ukiruhusu
kufanyika kwa shughuli za kilimo.
‘’Ukiangalia katika mji huu wa Arusha wananchi wengi wa hali ya chini na kati wanategemea kilimo kuendesha maisha yao lakini maeneo ya kilimo ni machache sana lakini mahusiano mazuri ya SUA na Jamii yamewezesha wananchi wengi kupata maeneo ya kulima mazao mbalimbali hasa mahindi, Maharage na mbogamboga ndani ya msitu huu kwenye maeneo ya wazi yaliyovunwa mbao na yenye miti midogomidogo iliyopandwa‘’ Alieleza Bi. Mami.
Kwa upande wake Mwananchi mwingine Julias Sumayaki Baada ya wazazi wake wote wawili kufariki aliachiwa wadogo zake watatu kuwatunza na kuwasomesha lakini hana kazi wala shamba ambalo anaweza kulima kutosheleza mahitaji yake na familia hiyo aliyoachiwa na wazazi wake.
‘’Sina neno zuri la shukrani ninaloweza kulisema kueleza furaha na shukrani zangu kwa uongozi wa SUA kutokana na msaada mkubwa tunaoupata baada ya kuturuhusu kupata kuni kwenye mabaki ya miti
ambayo imevunwa, Msitu huu sisi ndio maisha yetu mimi na wadogo zangu lakini na vijana wengi hapa mjini‘’ alisema bwana Sumayaki.
Aliongeza ‘’Kupitia msitu huu nimeweza kukata kuni za kutumia nyumbani na wadogo zangu lakini pia zingine kwenda kuuza Arusha mjini na kupata fedha ambazo zimeniwezesha kusomesha wadogo zangu nilioachiwa na wazazi wangu lakini pia kupata mahitaji yangu pale pale nyumbani, kwakweli huu msitu ni mkombozi ndio Baba na Mama wa familia yetu tulioachiwa na wazazi wetu‘.
Akizungumzia mchango huo wa Msitu wa Olmotonyi Meneja wa Kituo cha Mfunzo cha Msitu huo Bwana Said Kiparu amesema pamoja na kutoa nafasi kwa jamii inayozunguka msitu huo kupata kuni na maeneo ya Kilimo lakini Wananchi hao wamekuwa wakitoa ushirikiano mkubwa katika kutoa
taarifa mbalimbali za majingili wa msitu.
‘’Jamii inaona faida ya uwepo wa msitu huu na wanauona kuwa ni wa kwao kwakuwa tunawaruhusu kukata kuni hasa matawi kwenye maeneo ambayo tumevuna magogo ya mbao lakini pia tunapomaliza kuvuna wakati tunapanda miti mingine wao tunawapa nafasi ya kulima mazao madogo madogo hususani viazi mviringo, mbogamboga miti ikiwa midogo na wao wanashiriki kuitunza wanapohudumia mazao yao‘’ alifafanua Bwana Kiparu.
Nae Rasi wa Ndaki ya Misitu Wanyamapori na Utalii Dkt. Agnes Sirima amesema kuwapa Wananchi wanaozunguka Msitu wa Olmotonyi fursa ya kupata kuni na kulima ni mchango wa mzuri unaotolewa na Chuo kwa jamii kama majirani wanaozunguka msitu huo.
‘’Kwa namna hii ndio tunajenga mahusiano mema na jamii inayotuzunguka na kuwafanya wajifunze masuala ya umuhimu wa utunzaji misitu lakini pia kuwa walinzi wazuri wa msitu na hivyo kupunguza changamoto za uchomaji moto tofauti na ilivyo nyanda za juu kusini ambako majanga ya
moto huaribu sana misitu mingi ya kupanda na kuleta hasara kwa wahusika‘’ alieleza Dkt. Sirima.
Rasi huyo wa Ndaki amesema pamoja na kupata faida hizo lakini pia baadhi ya jamii inayozunguka msitu zimepata ajira na wengine hufanya vibarua mbalimbali ambavyo hupata fedha za kuendesha maisha yao huku wakijifunza pia hatua zote za upandaji, utunzaji, uvunaji nan a uchakataji wa magogo ya miti na kupata mbao.
Post A Comment: