Mashindano ya Kombe la Mkenda 2023 yamehitimishwa Juni 18, 2023 Wilayani Rombo Mkoani Kilimanjaro mshindi akiondoka na Kitita cha Shilingi milioni tatu.

Akizungumza mara baada ya mchezo wa fainali wa michuano hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Michezo Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo Ali Mayai amesema ameona kitu ambacho hakukitarajia kwani vijana walioshiriki katika fainali hizo wameonyesha vipaji vya hali ya Juu.
 
"Nimekiona kitu ambacho sikutarajia kabisa vijana wenye vipaji  na wanaocheza mpira wenye viwango vya juu, nimpongeze Mhe. Adolf Mkenda Mbunge kwa kuanzisha mashindano haya" amesema Ali Mayai

Mayai ameongeza kuwa  michezo kwa sasa si Burdani tu bali ni ajira na inachangia maendeleo kijamii na kiuchumi.

Mgeni Rasmi wa fainali za Mkenda Cup 2023, Naibu Waziri wa Mifungo na Uvuvi Mhe. David Silinde amesema mashindano hayo katika wilaya ya Rombo yamekuwa kivutio kikubwa na yameweza kuibua vipaji.

Silinde amewataka vijana wa Rombo kuendelea kujitokeza katika michezo kila mwaka ili kuendeleza vipaji vyao ambavyo vinaweza kugeuka ajira na kuwaletea maendeleo na kukuza uchumi wa wanarombo.

Naye mbunge wa Rombo Mhe. Adolph Mkenda amesema kuwa mashindano hayo yaliyoanza machi 18, 2023 yameshirikisha  timu 91 zilizohusisha vijana zaidi ya 2000 kutoka katika wilaya nzima ya Rombo.

Prof. Mkenda ameongeza kuwa mashindano hayo yameleta hamasa kubwa katika michezo  kama sehemu ya kukuza ajira na uchumi.

Katika fainali hizo timu ya Ubetu Kahe imetwaa ubingwa na kujinyakulia kitita cha shilingi milioni tatu pamoja na Kombe huku timu ya Kelamfua Mokala ikiibuka mshindi wa pili na kuondoka na kitita cha shilingi milioni mbili na mshindi wa tatu timu ya Rongai ikiondoka na shiling milioni moja

Viongozi mbalimbali wa Wilaya na Mkoa, wa Chama na Serikali wamehudhuria pamoja na  Wanamichezo  akiwemo Msimamizi Mkuu wa Digitali na Maudhui wa Yanga  Priva Abiud
Share To:

Post A Comment: