SERIKALI imepiga marufuku kwa taasisi yoyote ya Serikali kufunga biashara, ofisi ama maeneo yoyote ya uzalishaji kwa kigezo cha kukiuka taratibu mbalimbali.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba amesema wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Serikali Kuu bungeni mjini Dodoma kuwa kumekuwa na utaratibu unaochipukia kwa kasi wa taasisi mbalimbali za Serikali na Halmashauri kufunga biashara, ofisi na maeneo mengine ya uzalishaji baada ya kufanya kaguzi na kuthibitisha ukiukwaji wa sheria mbalimbali. “Ufungaji wa biashara, kwa sababu zozote zile, una athari kubwa kwa ustawi wa uchumi wetu kwa kuathiri ajira za wananchi, ustawi wa biashara, mapato ya kampuni na mapato ya Serikali. Aidha, utaratibu huu unakwenda kinyume na juhudi kubwa za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini. “Mheshimiwa Spika, ili kuondokana na athari hizo, napendekeza kuanzia tarehe 1 Julai 2023, iwe ni marufuku kwa taasisi yoyote ya Serikali kufunga biashara, ofisi ama maeneo yoyote ya uzalishaji kwa kigezo cha kukiuka taratibu mbalimbali,” amesema Waziri Mwigulu amependekeza sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zirekebishwe ili kumchukulia hatua mwenye biashara kwa makosa ya biashara na siyo kuifunga biashara yenyewe. Hatua hii inalenga kulinda ajira za watanzania, mapato ya biashara, kukuza uchumi na kuongeza mapato ya Serikali.
Post A Comment: