Na. Damian Kunambi Njombe.

Imeelezwa kuwa katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo halmashauri ya Wilaya ya Ludewa imepoteza jumla ya zaidi ya sh. Bil. 2 kilichosababishwa na majanga ya moto yaliyoteketeza misitu inayomilikiwa na halmashauri hiyo.

Hayo yameelezwa katika baraza la madiwani la halmashauri hiyo lililokuwa likijadili majibu ya hoja na mpango kazi wa utekelezaji wa hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ambapo majadiliano hayo yakiongozwa na mhasibu na mratibu wa hoja za CAG mkoa wa Njombe Lamsoni Ngambo huku mgeni rasmi akiwa mkuu wa mkoa huo ambaye aliwakilishwa na Katibu Tawala wa mkoa Judica Omary.

Akisoma taarifa ya hoja hiyo Ngambo amesema hekari 181za misitu zimeteketea kwa moto uliosababishwa na wananchi wanao jishughulisha na shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo katika maeneo jirani na misitu hiyo na kusababisha hasara ya kiasi hicho cha fedha kwa halmashauri hiyo.

" Wakulima wengi wamekuwa wakisafisha mashamba yao kwa kutumia moto pasipo kupata vibali maalumu vya uchomaji moto na kupelekea kuwasha moto pasipo utaalam na kusababisha majanga hayo ya kuchoma misitu". 

Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo mkaguzi ametoa ushauri kwa viongozi kutoa  elimu kwa wananchi juu ya utaalamu wa uchomaji mashamba sambamba na kuweka masharti ambayo yatatakiwa kufuatwa kwa wale wote watakaohitaji kuchoma mashamba yao.

Naye Mkaguzi Mkuu wa hesabu za nje Willy Undule amesema hasara hiyo ni kubwa hivyo ni vyema halmashauri hiyo ikaunda sheria ndogondogo ambazo zitawezesha kuwabana watu wanaojihusisha na uchomaji moto huo kwa makusudi.

" Unakuta mtu anawasha moto kwa kuwinda sungura porini pasipo kujua madhara anayo yasababisha ni makubwa kuliko hata thamani ya huyo sungura anayemuwinda". Alisema Undule.

Hata hivyo kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Judica Omary amemtaka Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Sunday Deogratias kuhakikisha wanaweka mkakati wa kuilinda misitu hiyo ili kuepuka kuendelea kupata hasa zaidi.

"Tunapo hamasishana kupanda miti tujitahidi pia kuweka mikakati ya kuitunza miti hiyo kwani inapotokea uharibifu kama huu huathiri misitu yetu na mapato yetu kama halmashauri" Alisema Judica.

Sanjari na hilo pia amewaagiza Madiwani kuungana na viongozi wa kata zao pamoja na halmashauri katika kusimamia vyema mapato ya Halmashauri ya wilaya hiyo kupitia kata zao ili waweze kutimiza lengo la makusanyo ya mapato kwa asilimia 100 kwani kuongeza kuwa mpaka mwishoni mwa mwezi mei mwaka huu Halmashauri hiyo tayari imekusanya mapato kwa asilimia 78 huku kwa mkoa mzima ikifikisha asilimia 92 hivyo wanapaswa kujitahidi kwa kipindi kilichobaki ili kukamilisha asilimia 22 iliyobaki.

Wise Mgina ni mwenyekiti wa Halmashauri hiyo pia ni Diwani wa kata ya Mundindi amesema kwa niaba ya baraza hilo amepokea maelekezo hayo huku akiwa na uhakika wa kukamilisha mapato hayo mapema iwezekanavyo.

" Tunafahamu  maeneo ya kuyapata mapato haya, hivyo tunahakika tutakamilisha asilimia 22 iliyosalia pasipo usumbufu wowote", Alisema Mgina.












Share To:

Post A Comment: