Na John Walter-Manyara
Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na
Maji (Ewura) imewataka wanafunzi wanaohitimu vyuo vya ufundi katika fani ya umeme kuwa na leseni
inayowatambua kulingana na viwango vyao.
Hayo yamesemwa leo Juni 5, 2023 na
Meneja wa Ewura Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Lorivii Long'idu wakati
akizungumza na wanafunzi wa masomo ya
umeme katika Chuo cha Ufundi Veta Manyara kilichopo mjini Babati, wakati wa
utoaji elimu maalum kwa wanafunzi hao juu ya umuhimu wa kuwa na leseni.
Amesema leseni hizo zina madaraja
tofauti na zinatolewa kwa kuzingatia ujuzi, elimu na uzoefu katika kufunga
umeme wenye msongo husika.
Mhandisi huyo amesema kutokana na
sera ya serikali ya kupeleka umeme vijiji vyote lakini pia wananchi na taasisis
mbalimbali kuendelea kujenga kila siku, kuna uhitaji mkubwa wa mafundi umeme.
Naye Mhandisi Tegemea Kamando,
amesema kuwa na leseni ni takwa la kisheria kifungu cha 5(a) cha Sheria ya
umeme Sura ya 131, ambacho kinaipa Ewura mamlaka ya kutoa leseni kwa watoa
huduma mbalimbali katika sekta ya umeme.
Mhandisi Kamando amesema wanatoa
leseni kwa waliohitimu mafunzo ya muda mfupi, diploma hadi digrii isipokuwa kwa
wafanyakazi wa TANESCO.
Akizungumza
kwa niaba ya mkuu wa chuo cha VETA Manyara, Msajili wa wanafunzi Sulpisi Awe
ameishukuru mamlaka hiyo kwa kuwaelimisha wanafunzi hao na kwamba
watakapohitimu wataweza kujiajiri na kuajiriwa bila vikwazo.
Mmoja wa wanafunzi hao, Israel Sebastian
amesema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa wa kutekeleza majukumu yao kwa
kuzingatia matakwa ha kisheria pindi wanapomaliza chuo.
Post A Comment: