Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ametoa onyo kwa Wafanyabishara wa Madini ya Jasi kufuata bei elekezi iliyopangwa na Serikali na kuacha kuwanyonya wachimbaji wa madini hayo.
Dkt. Kiruswa amesema hayo Wakati akifunga Kongamano la Chama cha Wanawake katika Sekta ya Madini 2023 (TWIMMI) lililofanyika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.
Aidha, Dkt. Kiruswa amewashauri wachimbaji wanawake wa madini nchini kutumia fursa zilizopo katika sekta hiyo kwa kushiriki moja kwa moja katika uchumi wa madini ili kuinua uchumi wao.
Pia, ameitaka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuwasaidi wachimbaji wa madini wa mkoa wa Lindi kwa kufanya tafiti katika maeneo ya uchimbaji madini kwa lengo la kuepuka uchimbaji wa kubahatisha.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack amemshukuru Dkt. Kiruswa kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika kilele cha kongamano hilo na amekishukuru chama hicho kuandaa kongamano hilo mkoani humo.
Sambamba na hayo, Tekack ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wachimbaji wote nchini kushiriki Kongamano la Madini la Mkoa wa Lindi linalotarajiwa kufanyika Juni 2023 mkoani humo.
Naye, Mkurugenzi wa Kanzidata wa GST, Terrence Ngole amewasisitiza wachimbaji wa madini wanawake kutumia taarifa za tafiti zinazotolewa na GST ili kuongeza tija na kuchimba kwa faida pasipo kubahatisha kwa lengo la kuongeza faida katika shughuli zao.
Kongamano hilo limeenda sambamba na maonesho ya madini ambapo zaidi ya wanawake 700 kutoka mikoa mbalimbali ya Kimadini nchini ikiwemo Dodoma, Kahama, Dodoma na Lindi wameshiriki.
Post A Comment: