SERIKALI imetoa zaidi ya shilingi bilioni 230 kutekeleza miradi mbalimbali ya kitaifa ya Barabara na madaraja mkoani Ruvuma Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma,Mhandisi Ephatar Mlavi amesema kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi bilioni 129 zimetumika kujenga Barabara ya lami nzito yenye urefu wa kilometa 66 kutoka Mbinga hadi Mbambabay wilayani Nyasa.


Amesema mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2018 kupitia kampuni ya China Henan International Cooperative Group ltd na ulikamilika mwaka 2021 hivyo kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji mkoani Ruvuma.

Ameutaja mradi mwingine ambao umekamilika kwa asilimia 100 kuwa ni wa ujenzi wa daraja la Mto Ruhuhu unaomwaga maji yake katika ziwa Nyasa ambapo serikali ilitoa shilingi bilioni 8.9 kujenga daraja hilo mradi ambao unaunganisha wilaya za Nyasa mkoani Ruvuma na wilaya ya Ludewa wilayani Njombe.

Mhandisi huyo wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma ameutaja mradi mwingine wa kitaifa kuwa ni ukarabati na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Songea ambao upo Ruhuwiko ambapo serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 37 kutekeleza mradi huo ambao unatumika na kutoa huduma zote. Hata hivyo amesema serikali ya Awamu ya Sita pia inatekeleza mradi wa ujenzi wa Barabara ya lami nzito kutoka Kitai hadi Lituhi ambapo kwa kuanzia mradi unatekelezwa kutoka Amanimakoro hadi Ruanda yenye urefu wa kilometa 35.

Amesema mradi unatekelezwa na na Mkandarasi Kampuni ya China Railway Seventh Group ambayo ilianza kutekelezwa Juni 2022 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2023 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 60. Hata hivyo amesema mradi wa Barabara Kitai hadi Lituhi sehemu ya Ruanda hadi Ndumbi yenye urefu wa kilometa 50 utahusisha ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami na kwamba zabuni imeshatangazwa na mradi unatarajia kuanza wakati wowote.

Akizungumzia mradi wa kitaifa wa ujenzi wa Barabara ya lami nzito kutoka Likuyufusi hadi Mkenda yenye urefu wa kilometa 60,Mlavi amesema mzabuni ameshatangazwa na serikali imetoa shilingi bilioni 60 kuanza kutekeleza mradi huo.

Mradi mwingine wa kitaifa unaosimamiwa na TANROADS ameutaja kuwa ni ujenzi wa Barabara ya Songea hadi Makambako kwa kiwango cha lami nzito sehemu ya Songea hadi Lutukira ikijumuisha sehemu ya Mtwara Korido mjini Songea yenye urefu wa kilometa 111.

Mhandisi Mlavi amesema serikali tayari imeshaingia makubaliano na mfadhili Benki ya Dunia kuanza kutekeleza mradi huo na kwamba hivi sasa mradi upo katika hatua za awali za manunuzi. Kulingana na Meneja huyo wa TANROADS mradi mwingine wa kitaifa unaosimamiwa na TANROADS ni ujenzi wa Barabara ya Lumecha,Londo hadi Kidatu mkoani Morogoro yenye urefu wa kilometa 512 ambao ukikamilika utaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Morogoro.

Amesema mradi huo upo katika hatua ya kupitia zabuni za wakandarasi na kwamba mradi utatekelezwa kwa kutumia mtindo wa usanifu ambapo utekelezaji wake unatarajia kuanza wakati wowote baada ya hatua za manunuzi kukamilika.


Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi akitoa taarifa ya mradi wa ukarabati na upanuzi wa kiwanja cha ndege Songea ambapo serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 37 kutekeleza mradi huo ambao umekamilika.

mradi wa ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 84 kutoka Kitai hadi Lituhi ambapo serikali inatekeleza sehemu ya kwanza kwa kujenga barabara ya lami kilometa 35 kutoka Kitai hadi Ruandamoja ya miradi mikubwa ya barabara ya lami nzito kutoka Mbinga hadi Mbambabay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma yenye urefu wa kilometa 66 ambapo serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 129 kutekeleza mradi huo uliokamilika kwa asilimia 100
Share To:

Post A Comment: