HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila imeendelea kuboresha huduma zake za kibingwa ya kibobezi ambapo hadi sasa imeweza kuwawekea puto (Intragastric ballon) wagonjwa 87, tokea kuanza kwa huduma hiyo hivi karibuni hapa nchini.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2022 na Mpango wa maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/24 upande wa Sekta ya Afya mapema leo Juni 15, Bungeni mjini Dodoma.
Ambapo ameeleza kuwa,Kuanza kutoa huduma hizo za kibingwa ya kibobezi ya puto, pia ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha upandikizaji viungo na ukarabati wa wodi za watoto mahututi (NICU) katika hospitali hiyo ya Taifa.
Aidha, katika hatua nyingine, amebainisha kuwa, Serikali imeendelea kuboresha huduma hizo nchini kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wake ambapo jumla ya wagonjwa 25 wamepatiwa huduma ya upandikizaji wa uroto katika hospitali za Muhimbili na Benjamin Mkapa.
"Upatikanaji wa huduma hii hapa nchini umepunguza gharama za kupata huduma nje ya nchi kutoka shilingi milioni 250 hadi kufikia milioni 70 sawa na punguzo la asilimia 72 ya gharama" Amebainisha Dkt. Mwigulu.
Aidha, Dkt. Mwigulu amesema kuwa, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kielelezo na ya kimkakati, kuimarisha sekta za uzalishaji ili kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi, kufungua fursa zaidi za ajira na maendeleo ya watu, kuboresha upatikanaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi zikiwemo huduma za afya.
Post A Comment: