SHIRIKA la Water Aid kwa ufadhili wa kampuni ya bia ya Serengeti Breweries limetoa mafunzo mbalimbali yakiwemo ya ujasiriamali na utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji kwa wanawake 24 wa Kijiji cha Kwamaizi katika Kata ya Kideleko wilayani Handeni mkoani Tanga.
Pamoja na mafunzo hayo wanawake hao wamepatiwa mafunzo yatakayowawezesha kutunza bwawa la maji ambalo linaendelea kujengwa katika Kijiji hicho ambalo limegharimu Sh.milioni 380 ambazo zimetolewa na Kampuni ya Bia ya Serengeti.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa ujenzi wa bwawa hilo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 90, Mkuu wa Miradi wa Water Aid nchini Tanzania Happiness Willbroad amesema katika kuhakikisha bwawa hilo linatunzwa wameamua kutoa mafunzo yatakayowezesha wananchi kuwa na uelewa wa kutosha kulitunza.
"Water Aid tumeamua kutoa mafunzo tofauti kwa wanawake hao wapatao 24 , lengo letu wawze kuwa wasimamizi wa hilo bwawa na kwa kusimamia hilo bwawa inamaanisha watakuwa wanalitunza kwa kupanda miti kwa kushiriki na wananchi wengine pamoja na Serikali ya Mtaa.
"Katika bwawa hilo kutapandwa miti ambayo itakuwa rafiki wa mazingira na utunzaji maji, lakini tunatarajia kwenye bwawa hilo utafanyika ufugaji samaki ,hivyo wanawake hao wamepatiwa mafunzo ya ufugaji samaki, hivyo watakuwa wakizalisha samaki na hivyo kuinua uchumi wao.
"Mafunzo hayo ambayo tumeyatoa tumefadhiliwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti katika kuhakikisha wanawake wa maeneo hayo wanapata mafunzo yaliyotolewa kwa siku nne na kisha kukabidhiwa vyeti na Mkuu wa Wilaya ili waanze kazi,"amesema.
Amefafanua zaidi lengo la mafunzo hayo ni kuona bwawa limeletwa lakini pia mwanamke aweze kunufaika kuipitia hilo bwawa kwa hiyo wamewapatia mafunzo ya Siku nne yanayohusu yanamasuala tofauti yakiwemo ya ujasiriamali,usafi wa mazingira na usafi binafsi, ukatili wa kijinsia, kutengeneza sabuni ,kutunza bustani, kufuga nyuki ili kupata asali pamoja na jinsi ya kuotesha samaki na kuhakikisha wanatunzwa
Kuhusu utunzaji bwawa hilo amesema wametoa mafunzo ya upandaji miti ambayo ni rafiki wa vyanzo vya maji ili yasikauke lakini kufyonza maji maeneo mengine na kuleta kwenye bwawa na jamii iweze kupata maji kwa muda mrefu zaidi.
"Lakini wawe sehemu ya kuhakikisha wanashiriki katika kulifanya bwawa kuwa safi na salama kwa mazingira ya binadamu kwani tunaamini kusipokuwa na matunzo mazuri bwawa hili linaweza kuwa chanzo Cha magonjwa kwa binadamu.'
Awali Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti Resper Hatibu amesema Kampuni yao imefadhili ujenzi wa bwawa hilo baada ya kuona wanayo sababu ya kurejesha maji kwa jamii huku akifafanua kutengeneza chupa moja ya bia inatumia maji lita tano ambayo ni mengi
"Hivyo tulikaa na kuangalia ni Kwa namna gani tutarejesha maji hayo kwa jamii ndipo tukaja na programu ya Water for Life ambayo imetuwezesha mpaka sasa kujenga mabwawa 24 Tanzania nzima.
Kwa upande wao baadhi ya Wananchi wametoa shukrani kwa wafadhili wa mradi huo Kwa kujenga bwawa hilo lakini wakati huo huo kupatiwa mafunzo ambayo yanakwenda kuboresha hali zao za maisha sambamba na kuondoa changamoto ya maji.
Mkazi wa Kijiji cha Kwamaizi Justine Kimea amesema wamesema wamekuwa na changamoto ya maji kwa muda mrefu kwani maji ambayo yalikuwa yanatoka yakitoka kwa mfano leo yanachukua mpaka miezi miwili ndio yanatoka tena hivyo kusababisha adha kwa wananchi.
Wakati Mkuu wa Wilaya ya Halmashauri ya Handeni Albert Msando amesema kasi ya ujenzi wa bwawa hilo inakwenda vizuri na kwamba kama halmashauri wamewezesha kupunguza gharama ya ujjenzi kwa kutumia vifaa ambavyo sio vya kukodisha.
Post A Comment: