Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Mohammed Mchengerwa, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mwongozo wa Usimamizi wa Hifadhi za nyuki katika hafla ya kufunga Maadhimisho ya Siku ya Nyuki yaliyofanyika Viwanja vya Bombadia mkoani Singida,May 21, 2023.Wengine kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dk.Ezekiel Mwakalukwa, Naibu Waziri wa wizara hiyo,Mary Masanja, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Singida, Lusia Mwiru.
Dotto
Mwaibale na Selemani Msuya, Singida
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Mohammed Mchengerwa amesema katika uongozi wake hatawavumilia
watendaji wazembe na wavivu, huku akitoa miezi miwili kwa watendaji wa sekta ya
misitu na nyuki, kuja na mpango mkakati wa ‘Achia Shoka Kamata Mzinga’ ambao
utawezesha uzalishaji wa asali nchini kuongezeka hadi kufikia tani
138,000.
Mchengerwa ameyasema hayo, May 21, 2023 katika hafla ya kufunga Maadhimisho ya Siku ya Nyuki yaliyokuwa yanafanyika katika Viwanja vya Bombadia mkoani Singida ambapo pia alizindua Mwongozo wa Usimamizi wa Hifadhi za nyuki, na vibanda maalum vya kuuzia asali pia ametoa Tuzo 5 za wadau wenye mchango mkubwa kwenye Sekta ya nyuki na ametoa vyeti kwa wanafunzi walioandika nsha nzuri kuhusu ufugaji wa nyuki.
Waziri huyo alisema iwapo
kuna watendaji ambao wanafanya kazi kwa mazoea na hawataki kubadilika,
hawatakuwa na nafasi katika uongozi wake.
Alisema iwapo kila
mtumishi akifanya kazi kwa bidii na kuachana na utendaji wa mazoea ni wazi kuwa
Tanzania itaweza kuzalisha zaidi ya tani 138,000 ya asali na kuondoka katika
tani 35,000 iliyopo sasa.
“Iwapo kila mmoja wetu
ataacha kufanya kazi kwa mazoea, wizara yetu itaweza kuchangia pato la taifa
kwa asilimia 30 hadi 50 na kuodoka kwenye asilimia 23. Niwaombe kwamba katika
uongozi wake uzembe na uvivu, sitaviruhusu, nataka kuona mipango ya ubunifu,
sio kuleta madokezo ya kutaka kusafiri nje ya nchi.
Nataka kuona ni namna
gani wizara hii itachangia kundi kubwa la vijana linaondoka katika dimbwi la
umaskini, mimi ni waziri mtendaji na tofauti, nataka matokeo, uadilifu na
uchapakazi, mheshimiwa naibu waziri kawaambie watendaji wabadilike,” alisema.
Waziri Mchengerwa alisema
taasisi zote za wizara zikitekeleza majukumu yake ipasavyo, Tanzania itapata
maendeleo ya haraka.
Alisema wizara hiyo
inasimamia asilimia 33 ya misitu, hivyo ni lazima tafsiri yake ionekane kwa
vitendo na kwamba kinyume na hapo, itawalazimu baadhi yao kuwapisha kwani
wameshindwa kuonesha walichoaminiwa nacho.
Mchengerwa alisema
Tanzania ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa asali Afrika na ya nne duniani, ila
matarajio yake ni kuona inakuwa ya kwanza duniani kwa kuwa ina rasilimali
misitu mingi ambayo inaweza kuzalisha zao hilo.
Alisema asali ya Tanzania
ina soko kubwa ndani na nje ya nchi, hivyo hakuna sababu ya kushindwa kutumia
fursa hiyo muhimu.
“Kauli mbiu ya Siku ya
Nyuki mwaka huu inasema ‘Tuwalinde Nyuki kwa Ustawi wa Mazingira na Usalama wa
Chakula, inaakisi kuwa tafiti zinaonesha asilimia 80 ya chakula kinatokana na
uchavushaji wa nyuki,” alisema.
Aidha, Waziri huyo
ameilekeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kuhakikisha maeneo yenye
uoto wa misitu, yanatambuliwa na kuhifadhiwa, wananchi wanapata elimu ya
uhifadhi na ufugaji kibiashara na vijiji vyote viwe na mpango bora wa matumizi
ya ardhi.
Pia aliitaka TFS kuandaa
maeneo ambayo yatatumika kufuga nyuki kwa njia ya kiutalii, ambapo amewataka
waende kujifunza nchini Slovenia namna ambavyo wananufaika na utalii wa nyuki.
Kwa upande wake Kamishna
wa Uhifadhi TFS, Profesa Dos Santos Silayo, alisema wakala hiyo imejipanga
kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Waziri Mchengerwa, ili kuhakikisha sekta
hiyo inachangia ukuaji wa uchumi.
Alisema TFS imekuwa
ikitoa elimu kwa umma kuhusu ufugaji nyuki wa kisasa, ambapo kwa mwaka
wawanatumia tkaribani milioni 90 kuhakikisha asali ya Tanzania inapata ithibati
ya kuuzwa soko la dunia.
“Sisi kwa kushirikiana na
wadau wa nyuki tutahakikisha mnyororo wa thamani wa mazao ya nyuki unaongezeka,
ili mchango wa wizara hii uweze kuongezeka,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,
Thomas Apson ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba,
alisema mkoa huo umepata mafanikio kupitia ufugaji wa nyuki ambapo zaidi ya
wananchi 12,133 wanajihusisha katika eneo lenye ukubwa wa hekta 476,361 za
misitu ya asili na vichaka vya Itigi.
“Ufugaji wa nyuki umeingiza shilingi 890 zilizotokana na uzalishaji wa asali tani 89 na tani 20 za nta, hivyo tunaamini zao hili ni muhimu katika mkoa wetu. Ila uzalishaji huu unabeba kauli mbiu yetu ya Achia Shoka, Kamata Mzinga,” alisema.
Vijana wa Skauti wakifanya itifaki ya kumvika skafu, Waziri wa Maliasili Dk. Mohammed Mchengerwa baada ya kuwasili kufunga Maadhimisho ya Siku ya Nyuki mkoani Singida.
Waziri wa Maliasili Dk. Mohammed Mchengerwa (kulia) akivuta pazia kuachiria uzinduzi wa kibanda maalumu cha kuuzia mazao ya nyuki ikiwemo asali.
Post A Comment: