Na. Damian Kunambi, Njombe.


Wakazi wa kijiji cha Kiyogo Kata ya Masasi Wilayani Ludewa Mkoani Njombe wametakiwa kuunda kikundi cha ulinzi shirikishi(Sungusungu) ili kukomesha matukio ya wizi pamoja na matukio ya mauaji ambayo yamekuwa yakijitokeza kijijini hapo.

Akizungumza hayo katika mkutano wa hadhara na wanakijiji hao Mkuu wa Polisi wilayani Ludewa Deogratius Massawe mara baada ya kuwasili kijijini hapo akiwa na Mkuu wa dawati la jinsia la Polisi Violet Gideon kwa lengo la kutoa elimu ya kupinga ukatili, wizi na masuala ya ushirikina baada ya wananchi kulalamikia kukithiri  kwa matukio hayo.

Afande Massawe amesema kabla ya kufikiria polisi wananchi wanapaswa kuimarisha ulinzi wao wenyewe kwa kuunda vikundi hivyo ambapo kila kaya atatakiwa kutoka mtu mmoja mwenye nguvu na kuungana kisha kuzunguka katika maeneo mbalimbali ya kijiji hicho.

" Najua mko mbali na kituo cha Polisi, hivyo nanyi mnapaswa kusaidiana na polisi katika kuimarisha ulinzi na hii itawasaidia kupunguza matukio haya ya uhalifu mnayo yalalamikia" Amesema Afande Massawe.

Aidha kwa upande wake Mkuu wa dawati la jinsia Violet Gideon amewataka wananchi hao kuacha tabia ya kuhifadhi video za ngono ama zisizo na maadili kwenye simu kwani watoto wamekuwa wakichezea simu hizo na kuzitazama video hizo chafu baada ya hapo wanaanza kutaka kufanya majaribio.

" Walindeni watoto wenu kwa kuepuka mazingira ambayo yanaweza kuwa sababu ya kuharibikiwa kwa watoto wetu, mambo haya ya utandawazi umekuja na vitu vingi vya kujenga na kubomoa pia hivyo tuweni makini katika hilo". Amesema Afande Violet.

Hata hivyo kwa upande wa wananchi wa kijiji hicho cha Kiyogo wameonyesha kuipokea vyema elimu hiyo huku wakiwapongeza viongozi hao wa Polisi kwa kufika kijijini hapo kwani tangu kuanzishwa kwa kijiji hicho hawajawahi kutembelewa na polisi na kuwapa elimu.

"Tunawashukuru sana kwa kufika huku kijijini kwetu na kutupa elimu hii ambayo awali hatukuwahi kuipata, tumezoea kuona Polisi wakija katika kamata kamata ama matukio mbalimbali lakini si kirafiki kama hivi, kiukweli tumejifunza kitu kikubwa sana". Jacob Mahundi, mmoja wa wanakijiji.

Share To:

Post A Comment: