Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Itigi, Benjamin Masangula, akizungumza na mabalozi wa kata hiyo katika kikao kazi kilichofanyika juzi mjini humo. Wengine waliokaa meza kuu kutoka kushoto ni Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Samson Sirilo na Diwani wa Kata hiyo, Ally Minja.
...........................................
Na Dotto Mwaibale, Itigi
VIONGOZI wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Kata ya Itigi mkoani Singida
wamekutana na mabalozi wa kata hiyo kwa ajili ya kupanga mikakati ya utendaji
wa kazi ili kuendelea kuisukuma mbele kata hiyo kimaendeleo.
Akizungumza katika kikao kazi hicho, Afisa
Mtendaji wa kata hiyo Saimon Sirilo alisema wamekutana na mabalozi 56 wa Kata
ya Itigi mjini ili kupanga mikakati nao ya kusukuma maendeleo ya kichama na
Serikali.
" Mabalozi ni kundi muhimu sana katika jamii
hasa katika kutekeleza majukumu ya chama na Serikali kutokana na kuwa jirani na
wananchi tofauti na makundi mengine," alisema Sirilo.
Alisema pamoja na kukao nao katika kikao hicho
lengo kubwa lilikuwa ni kuwatia moyo kutokana na mchango wao mkubwa katika
jamii ili waendelee kuwa na ari na moto wakuchapa kazi kutokana na kutegemewa
na chama, Serikali na Taifa kwa ujumla.
Katibu wa CCM wa Kata hiyo, Benjamin Masangula
akizungumza kwenye mkutano huo alisema kundi hilo la mabalozi ni la muhimu
kwani wamekuwa wakichochea maendeleo ya wananchi katika nyanja zote mbili za
kisiasa na Serikali na kwa kulitambua hilo wameamua kuwalipia ada za uanachama mabalozi wote 56 kwa mwaka
mzima.
"Mchango wa kundi hili ni mkubwa sana
hatuwezi kuwatenga, chama na Serikali ni kama ulimi na mate tumeamua kuwatia
moyo kwa kuwalipia ada za uanachama jambo ambalo lipo ndani ya uwezo
wetu," alisema Masangula.
Aidha, Masangula alisema wametoa kadi 100 ambazo
zimetolewa kwa mabalozi hao kwa ajili ya kwenda kuwatafuta wanachama wapya wa
chama hicho katika maeneo wanayotoka na kuwa mpango huo utakuwa ni endelevu
wenye lengo la kukihimarisha chama kwa kupata wanachama wengi zaidi.
Katika mkutano huo viongozi wengine waliohudhuri
ni Diwani wa Kata ya Itigi, Ally Minja ambaye aliomba kuendelea kudumisha
ushirikiano baina ya Serikali, chama na kundi hilo la mabalozi kwa mustakabari
mzima wa maendeleo ya kata hiyo.
"Maendeleo ya kata yetu yataendelea kuwa juu iwapo tutadumisha upendo, mshikamo na kushirikiana sisi sote pamoja na wananchi wetu tunaowaongoza na si vinginevyo," alisema Minja
Post A Comment: