Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kilimanjaro, umewataka viongozi wa ngazi za vitongoji, vijiji na Kata, kuitisha mikutano ya wananchi ili kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili na kuhakikisha zinatafutiwa ufumbuzi.

Rai hiyo imetolewa na mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, Ivan Moshi wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Mabogini, Wilaya ya Moshi, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kamati ya utekelezaji ya umoja huo, kukutana na makundi mbalimbali na kufanya mikutano ya wananchi kusikiliza kero.

“Wenyeviti wa vitongoji, vijiji  na hata madiwani, tunataka kuwaona mkiitisha mikutano kusikiliza kero na changamoto za wananchi, na katika mikutano hiyo watendaji wa serikali waliopo katika maeneo yenu wakiwemo watendaji wa vijiji, kata na wataalamu mbalimbali, wafike kujibu na kueleza namna serikali imejipanga kushughulikia hayo” amesema Moshi.

“Hatutaki longolongo kwenye kutimiza majukumu ya kutumikia wananchi, na hatutaki viongozi wa kukaa ofisini kuzunguka na viti, kila mmoja atimize wajibu wake, kwani 2020 tulikuja kwa wananchi kunadi ilani yetu ya uchaguzi, yapo mengi ambayo tuliahidi kuyatekeleza, sasa ni jukumu lenu viongozi ambao mmepewa dhamana, kufika kwa wananchi kuwaeleza ni yapi yamefanyika na ni upi mpango katika kutekeleza yale ambayo hayajafanyiwa kazi,”ameongeza.


Akizungumza katika mkutano huo, mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Moshi vijijini, Yuvenal Shirima ameomba vijana wanapojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupewa nafasi ili kutumika kikamilifu katika taifa.


“Tunao vijana ambao ni mahiri na wenye uwezo wa kuongoza katika nafasi mbalimbali kuanzia ngazi za vitongoji, vijiji na nafasi nyingine, itakapofika wakati wakaomba nafasi na tukawapima na kuona wanafaa, naomba tuwape kipaumbele wakaonyeshe umahiri wao katika utendaji na kuwezesha Taifa kusonga mbele,” amesema Shirima.

Shirima amewaomba wenyeviti wa vijiji ambayo vina mashamba, kutoa mashamba hayo kwa vijana, ili yakatumike katika kilimo bora na chenye tija, hatua ambayo itachochea ukuaji wa uchumi kwa vijana na taifa kwa ujumla.

Kamati ya utekelezaji ya UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro, ipo katika ziara ambapo inakutana na makundi mbalimbali ya vijana ikiwemo vijana wa bodaboda na bajaji na mikutano ya hadhara kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili, na katika Wilaya ya Moshi vijijini, pia walipokea wanachama wapya wa jumuiya hiyo na kukagua ujenzi wa nyumba ya mtumishi.

Share To:

Post A Comment: