Na; Mwandishi wetu, Dodoma

Akifungua kikao cha tathmini kilichowakutanisha wadau mbalimbali Jijini Dodoma katika Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu chini ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) Nchini, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Kaspar Mmuya amesema kuwa mkakati wa Serikali katika muktadha wa Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu unahusisha kuzuia utekelezaji wa makosa haya ikiwa ni pamoja na kuwafungulia mashtaka wahalifu kwa mujibu wa Sheria na kuwasaidia wahanga.

Katibu Mkuu Mmuya amesema kuwa namna bora ya kupambana  kimkakati na uhalifu huu ni kuhakikisha jamii inabadilishwa mtazamo na kuona kuwa jambo hilo sio sahihi  kwa kuwa na mifumo sahihi , kusimamia sheria ,kanuni na miongozo.

“Sisi peke yetu hatuwezi kufanikisha haya kama Watunga Sera, Sheria ambao ni Waheshimiwa Wabunge hawana elimu kuhusu Usafirishaji Haramu wa Binadamu. Niagize elimu kuhusu Usafirishaji Haramu wa Binadamu itolewe kwa Wabunge kwani ndio wasemaji wazuri sana wanaotutetea katika ngazi ya jamii ambako ndipo tatizo lilipo wale wakisema kwa kulikemea kwa kuelewa wakalimiliki kuwa ni tatizo tunaweza kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine.”alisema Mmuya

Mmuya amesema  katika tathmini ya utekelezaji wa mpango kazi wa Kitaifa wa Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu ni vyema taarifa itakayowasilishwa iweze kujibu baadhi ya maswali aliyoyaainisha ikiwa ni pamoja na kazi zilizotekezwa zilizosaidia katika kuzuia uhalifu huo na kwa kiwango gani,upepelezi na ukamataji wa uhalifu umefanyika kwa kiwango gani, hatua zilizochukuliwa, kubainisha mikakati iliyopangwa na malengo yaliyofikiwa.
 
Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) Nchini, Maurizio Busatti amesema kuwa IOM imekuwa ikishirikiana na Serikali na Mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kutekeleza mpango kazi juu ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mapambano hayo

Busatti ameongezea kuwa ni wakati sasa Tanzania kuvuka mipaka kuangalia mienendo muhimu ya Kikanda na Kidunia ili kuweza kuioanisha Tanzania na viwango bora vya Kimataifa vya kukabiliana na Biashara Haramu ya Binadamu.








Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: