Afisa Kodi wa Mamlaka  ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Singida, Hashim Mkwayu akizungumza na mawakala wa mabasi Stendi Kuu ya Mabasi Misuna wakati akitoa elimu kuhusu umuhimu wa  kutoa risiti za kielektroniki kwa abiria wakati wa kampeni maalum iitwayo Tuwajibike ilioanza May 9, 2023 na kuwalenga wafanyabiashara wote.

Na Dotto Mwaibale, Singida. 

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Singida imeendesha kampeni ya Tuwajibike yenye lengo la kuwataka wafanyabiashara na mawakala wa mabasi kutoa risiti za kielektoniki (EFD) wanapouza bidhaa zao na kuwakatia tiketi abiria wao chini ya kauli mbiu isemayo ukiuza toa risiti na ukinunua dai risiti.

Akizungumza na mawakala wa mabasi Stendi Kuu ya Mabasi Misuna Afisa Kodi wa TRA, Hashim Mkwayu alisema lengo la kampeni hiyo imelenga utoaji wa elimu kwa mawakala wa mabasi kuhusu umuhimu wa  kutoa risiti za kielektroniki kwa abiria na kuwahimiza abiria wao kuhakikisha wanadai risiti tofauti na hapo watatozwa faini.

Alisema TRA mkoani hapa haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria mawakala wa magari ya usafirishaji abiria ambao watabainika kutotoa risiti hizo kwa abiria na abiria ambaye atashindwa kudai risiti.

Alisema adhabu hiyo pia itawahusu mawakala ambao watashindwa kutoa risiti kwa mizigo yote itakayokuwa inasafirishwa kwenye magari hayo.

Alisema kampeni hiyo pia itawahusu wafanyabiashara wote wenye maduka yanayouza bidhaa mbalimbali, maduka ya dawa, vipodozi, chakula, wauza nyama (bucha) mahoteli, nyumba za kulala wageni, vifaa vya ujenzi nguo na nyingine zote.

Aidha, Mkwayu alisema TRA itawachulia hatua mawakala wanaokatisha tiketi katika vituo visivyo rasmi (Vituo Bubu) ambao wanatoa risiti zisizo za kielektroniki kwani kwa kufanya hivyo wamekuwa wakiikosesha Serikali mapato.

Hatua hiyo imekuja kufautia malalamiko kutoka kwa baadhi ya mawakala hao kuhusu kuwepo kwa vituo  bubu ambavyo vinasababisha mkanganyiko wa bei wakati wa kuwaandikia risiti za kielektroniki abiria ambao wameandikiwa tiketi za kawaida na kupelekea kutozwa faini.

Wakala wa mabasi hayo Ibrahimu Abdul alisema vituo hivyo bubu vimekuwa ni changamoto kubwa kwao na akaomba vyombo husika Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), TRA. Polisi na Manispaa ya Singida wakae pamoja kutafuta njia ya kuiondoa.

" Nia ya Serikali ya ukusanyaji wa mapato ni   njema kwani fedha zinazopatikana ndio zonazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, kulipa mishahara, kununua madawa na vifaa tiba na mambo mengine sasa haiwezekani kukawa na watu wachache wanao tuharibia kazi kwa kukwepa kulipa kodi kwa njia za ujanja ujanja," alisema Abdul.

Afisa Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA Mkoa Singida Swaumu Mvungi alisema mamlaka hiyo itaanza kuyafuatilia maeneo yote ambayo sio rasmi yanayotumika kama vituo vya magari na kutoa risiti ambazo sio za kielekitroniki.

Alivitaja vituo hivyo kuwa ni Sabasaba, Jovena, Namfua na Msufini na akatoa onyo kwa mawakala wanaofanya hivyo kuacha mara moja kabla ya kufikiwa na mkono wa sheria na kuwa kampeni hiyo inafanyika katika wilaya zote mkoani hapa ambazo ni Mkalama, Iramba, Singida Manispaa,Ikungi Manyoni, Itigi na Singida DC..

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Mabasi Mkoa wa Singida, Musafiri Ramadhani alisema jambo la kuondoa vituo bubu hivyo liangaliwe kwa mapana kwani ni changamoto kubwa kwao.

Wakala Patrick Mgimbwa alisema jambo hilo lisifanyiwe masihara wala kufanywa la kisiasa kwani mawakala hao wa vituo bubu wamekuwa wakitoza nauli watoto wa jamii ya kifugaji hadi Sh.50,000 kutoka Singida hadi Dar es Salaam na kuwa wizi huo wa mchana kweupe umepewa jina la 'Abiria zawadi ya Mungu,

Kwa upande wake Wakala Athumani Kimwanga aliwaomba TRA wapite katika maeneo yote vilipo vituo bubu hivyo wakiwa wamevaa nguo za kawaida na kufanya uchunguzi hata kwa kujifanya ni abiria watabaini hayo yanayolalamikiwa na kuweza kuvikomesha vitendo hivyo.

Baadhi ya mawakala wa mabasi Mkoa wa Singida wakipata elimu hiyo iliyokuwa ikitolewa na maafisa wa kodi wa TRA (hawapo pichani)
Maafisa wa TRA waliokuwa kwenye kampeni hiyo. Kutoka kulia ni Victor Mbwambo, Hashim Mkwayu, Benedict Moshi, Swaumu Mvungi na Wilson Bamale.
Maafisa hao wa TRA wakitoa elimu hiyo kwa mfanyabiashara wa duka la vipodozi lililopo maeneo ya  soko kuu mjini hapa.
Afisa Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  Mkoa Singida Swaumu Mvungi akizungumzia kampeni hiyo ambayo ni ya muhimu sana katika kukusanya mapato ya Serikali.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Mabasi Mkoa wa Singida, Musafiri Ramadhani, akizungumza wakati mawakala hao wakipewa elimu hiyo.
Afisa Kodi wa Mamlaka  ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Singida, Hashim Mkwayu, akibandika nje ya duka kipeperushi kinachozungumzia kampeni hiyo.
Wakala Issa Hussein Nandi akichangia jambo wakati wa kupata elimu hiyo.
Wakala, Ibrahim Abdul akizungumza wakati wa kutolewa kwa elimu hiyo.
Maafisa wa TRA Mkoa wa Singida, wakitoa elimu hiyo kwa mawakala wa mabasi.
Wakala Patrick Mgimbwa akizungumza changamoto waliyonayo kuhusu vituo bubu vinavyotumika kutumika kukatia tiketi abiria kinyume na taratibu.
Wakala Athumani Kimwaga, akichangia jambo wakati elimu hiyo ikitolewa.
 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: