Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi.
Mtandao wa Polisi Wanawake mkoa wa Arusha (TPF Net) leo Mei 07, 2023 umesherehekea siku ya akina mama duniani kwa kutoa elimu ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watu waliojitokeza kusherehekea siku hiyo.
Akiongoza kutoa elimu hiyo Mwenyekiti wa Mtandao huo mkoani Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Edith Swebe amesema mbali na kushiriki michezo mbalimbali iliyoandaliwa pia wametumia siku hiyo kupinga na kukemea vitendo vya ukatili katika jamii.
Sambamba na hilo pia amebainisha kuwa wametumia siku hiyo kuhamasishana kushiriki mkutano wa Kimataifa utakaowakutanisha Polisi wanawake toka nchi mbalimbali utakaofanyika jijini Dar es Salaam.
Awali akitoa elimu kuhusu ukatili Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto mkoani humo Mrakibu msaidizi wa Polisi ASP Happiness Temu amesisitiza wazazi kuchukua jukumu lao la malezi bora kwa watoto ili kupunguza ama kumaliza vitendo vya ukatili katika jamii.
ASP Temu amesema wazazi wanaowajibu mkubwa wa kuhakikisha wanakua karibu na watoto wao kwa kusikiliza changamoto zao, kufuatilia mienendo yao ya kila siku pamoja kuwaonya ama kuwaadhibu pale wanapokosea badala ya kuwaacha bila uangalizi.
Pia amekemea tabia ya baadhi ya wazazi kukaa meza ya maridhiano na kumaliza kesi za ukatili hususani kwa watoto pindi zinapotokea badala ya kuripoti katika vyombo vya sheria hali inayopelekea kuongezeka kwa matukio ya ukatili katika jamii.
Tukio hilo limefanyika ikiwa ni mkakati wa Jeshi la polisi mkoani humo la kuhakikisha wanayafikia makundi yote katika jamii kwa kutoa elimu, kukemea pamoja na kupinga vitendo vyote vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Zaidi ya Wanawake elfu moja toka taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi wameshiriki katika tukio hilo ambalo limefanyika katika viwanja vya ofisi ya Mkurugenzi wilaya ya Arusha.
Post A Comment: