Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) leo Mei 08, 2023 jijini Dodoma imefanya semina na Kamati ya kudumu ya Bunge ya uwekezaji wa mitaji ya Umma juu ya Usimamizi wa Pori la Akiba Kilombero


Semina hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Bunge, Jengo dogo la utawala Chumba No. 49 imelenga kuieleza Kamati ya kudumu ya bunge juu ya umuhimu wa Pori la Akiba Kilombero, changamoto zinazokabili Pori hilo na namna TAWA ilivyojipanga kukabiliana na changamoto hizo.

Akizungumza wakati wa kutoa wasilisho mahsusi la Pori la Akiba Kilombero, Kamishna wa Uhifadhi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Joas Makwati amesema Pori hilo lina umuhimu mkubwa Kwa Taifa kwani linachangia asilimia sitini na 65 (65%) ya maji kwenye bwawa la Mwalimu Nyerere (JHPP) ambayo yanatarajia kuzalisha Megawati 2, 115 za umeme utakaotumika majumbani, viwandani na kwenye shughuli za usafirishaji (reli na magari).

Sambamba na faida hiyo, Pori hilo limedaiwa kuwa chachu ya kufungua fursa za Utalii ikiwemo shughuli za Uwindaji wa Kitalii ambazo zinaongeza fedha nyingi za kigeni ikizingatiwa kuwa mpaka sasa Pori la Akiba Kilombero lina Vitalu vinne vya Uwindaji wa Kitalii

Makwati amesema katika kipindi cha Mwaka 2016/17 hadi 2020/21 TAWA ilitoa jumla ya Shillingi 425, 221,402 Kwa Halmashauri za Wilaya ya Kilombero, Ulanga na Malinyi kama gawio la 25% ya mapato yatokanayo na shughuli za Utalii katika Pori la Akiba Kilombero.

Pamoja na faida zingine, Joas Makwati amesema TAWA imetoa fursa Kwa wananchi kufanya shughuli za uvuvi Kwa utaratibu Maalumu katika Pori hilo, jambo ambalo limewanufaisha sana wakazi Kwa Kilombero na Mkoa wa Morogoro Kwa ujumla

Akibainisha changamoto za Pori hilo, Kamishna wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Joas Makwati amesema Pori la Akiba Kilombero linakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi ambapo Kwa sasa Kuna jumla ya watumishi 88 kati ya watumishi 279 wanaohitajika.

Changamoto zingine zilizobainishwa ni ukosefu wa miundombinu, vikwazo katika kutekeleza kazi za himasheria kutokana na Kijiji Cha Ngombo na vitongoji 14 vya Vijiji vingine kuwemo ndani ya Pori hilo pamoja na kutotekelezwa Kwa sheria ya mpango wa matumizi ya ardhi ya Mwaka 2007.

Akieleza hatua za kukabiliana na changamoto hizo, Makwati amesema TAWA imeandaa mpango shirikishi wa Miaka mitatu (2023 - 2025) wa Usimamizi wa Pori hilo utakaohakikisha ulinzi, uhifadhi, na matumizi endelevu ya rasilimali ya maji na Wanyamapori unafanikiwa.

Hatua nyingine zilizochukuliwa na TAWA ni pamoja na kuboresha miundombinu Kwa Kuweka alama za mpaka ambapo jumla ya vigingi 301 kati ya 1, 686 vimewekwa, ujenzi wa kambi mbili za doria, kutoa elimu ya Uhifadhi Kwa wananchi 9, 861 wa Vijiji 16 katika Wilaya za Kilombero, Malinyi na Ulanga

Pia TAWA imeongeza vitendea kazi (gari 05, boti 04, trekta 02, na pikipiki 02), imeanzisha Kanda mbili za kiutawala Ili kuimarisha ulinzi na kurahisisha utoaji huduma Kwa wananchi na Usimamizi wa Pori
n.k

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Anderson Mutatebwa ametoa ufafanuzi wa kisera kuhusu tathmini inayofanywa na Serikali Kwa wananchi wa Kijiji Cha Ngombo na Vitongoji vilivyopendekezwa kuondolewa nje ya hifadhi.

Kipee ameipongeza Kamati Kwa maelekezo na Ushauri walioutoa na akiahidi kuwa Serikali imeyapokea na itayafanyia kazi.

Akitoa Ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyoibuiliwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo, Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda amesema kuhusu suala la matumizi bora ya ardhi, utekelezaji wake unahitaji ushirikishwaji wa kutosha kwani ni suala mtambuka ambalo litahusisha Wadau mbalimbali na sekta za Serikali ikiwemo Wizara ya TAMISEMI, na ameomba kuongeza umoja na mshikamano katika suala hilo Ili kuhakikisha jam
bo hilo linafanikiwa.

Pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa kuridhia kuanzisha Pori la Akiba Kilombero na kuahidi kushirikiana na Wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kamati za Bunge, wabunge wa maeneo husika, Serikali za Mkoa na Wilaya, pamoja na Wananchi Ili kufikia malengo ya Uhifadhi endelevu Kwa manufaa ya jamii na Taifa Kwa ujumla.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa mitaji ya Umma ambaye pia alikuwa Mwenyekiti katika Semina iliyofanyika Leo, Bw. Augustino Vuma ameeleza kufurahishwa kwake na wasilisho la Pori la Akiba Kilombero na kusema kuwa Kamati imelielewa na hivyo watajitahidi Kuonesha ushirikiano wao kwa TAWA Ili kuhakikisha inaendelea kulinda mazingira na rasilimali zilizopo ndani ya hifadhi hiyo Kwa manufaa ya Taifa.








Share To:

Post A Comment: