Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema katika mwaka 2022/23, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC)limekamilisha hatua za ununuzi na kumpata Mzabuni wa kujenga boti moja (1) ya matibabu (Ambulance Boat) na boti mbili (2) za Utafutaji na Uokoaji zitakazotumika katika Ziwa Victoria ambapo kwa sasa Taarifa ya Uchambuzi wa Zabuni imewasilishwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ridhaa.
Mbarawa ameyasema hayo wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wakati akiwakilisha Bajeti ya Wizara hiyo ya mwaka 2023/2024.
Amesema kuwa Katika kusimamia vyema Udhibiti wa Huduma za Usafiri kwa njia ya Maji TASAC imeshamkabidhi Mkandarasi eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo Kikuu cha Uratibu wa shughuli za Utafutaji na Uokoaji (Maritime Rescue Coordination Centre – MRCC) cha kikanda kitakachojengwa eneo la Ilemela Mwanza.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha Bungeni mpango wa Makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/24 ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Mbarawa amesema TASAC inaendelea pia na mchakato wa kuanza ujenzi wa vituo vidogo vitatu vwa utafutaji na uokoaji.
“Mkandarasi amepatikana kwa ajili ya kujenga vituo vingine vidogo vitatu (3) vya Utafutaji na Uokoaji (Search and Rescue Stations – SARS) katika maeneo ya Kanyala - Geita, Nansio - Ukerewe na Musoma – Mara na sasa amekabidhiwa maeneo ya ujenzi na anaendelea na maandalizi ya awali, amesema Mhe. Mbarawa.
Kazi ya ujenzi wa Kituo Kikuu cha Uratibu wa shughuli za Utafutaji na Uokoaji (Maritime Rescue Coordination Centre – MRCC) itakamilika ndani ya miezi 18 na Kituo cha Utafutaji Kanyala - Geita, Nansio - Ukerewe na Musoma – Mara inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12.
Post A Comment: