Katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mtandao wa barabara za vijijini na mijini kwa Mkoa wa Mwanza zimeimarika maradufu.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Goodluck S. Mbanga anasema hatua hii imetokana na uamuzi wa dhati wa Rais Samia wa kuongeza bajeti kwa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Mwanza kwa zaidi ya asilimia 100.
Mkoa wa Mwanza una mtandao wa barabara zinazosimamiwa na TARURA zenye jumla ya urefu wa kilomita 8586.764, kati ya hizo kilomita 95.18 sawa na asilimia 1.11 ni za lami, kilomita 9.555 ambazo ni sawa na asilimia 0.11 ni za zege huku kilomita 16.679 sawa na asilimia 0.19 ni za mawe, kilomita 1823.092 sawa na asilimia 21.23 za changarawe na kilomita 6642.257 sawa na asilimia 77.35 ni barabara za udongo.
Aidha, barabara zenye hali nzuri ni kilomita 2,498.951 ambazo ni sawa na asilimia 29.10 huku barabara zenye hali yakuridhisha ni kilomita 3647.645 sawa na asilimia 42.48 wakati zile zilizoko katika hali isiyoridhisha ni kilomita 2,440.168 sawa na asilimia 28.42.
Pia, Mkoa wa Mwanza una jumla ya madaraja 55, maboksi kalavati 336, makalavati madogo 4500 na drifti 182.
Anapozungumzia mafanikio ya miaka miwili ya Mheshimiwa Rais Samia, Mhandisi Mbanga anasema kumekuwa na ongezeko la bajeti kubwa la bajeti ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara za wilaya zinazohudumiwa TARURA Mkoa wa Mwanza kuliko iliyokuwa ikitengwa kabla ya kuingia madarakani kwa uongozi wa awamu ya sita
Fedha hizo ni kutoka kwenye vyanzo vitatu vya mapato ambavyo ni fedha za jimbo, tozo ya mafuta na mfuko wa barabara.
Anasema kwa mwaka 2020/21 mtandao wote wa barabara za Mkoa wa Mwanza kwa barabara za wilaya zote nane ilitengwa takribani Sh bilioni 10.189 na kwa mwaka 2021/22 zilitengwa zaidi ya Sh bilioni 26.339.
“Kwa mwaka wa fedha 2022/23 barabara za wilaya zinatohudumiwa na TARURA Mkoa wa Mwanza zilitengewa takribani Sh bilioni 25.727,” anasema.
Anasema hatua ya kuwapo kwa ongezeko la bajeti kumechangia ongezeko la kilomita za barabara za lami, zege, mawe na changarawe ndani ya miaka miwili ya uongozi wa awamu ya sita.
Akifafanua zaidi Mhandisi Mbanga anasema barabara za lami zimeongezeka kutoka kilomita 72.898 hadi kufikia kilomita 95.18 wakati kwa barabara za zege zimeongezeka kutoka kilomita 4.801 hadi kufikia kilomita 9.555.
Anasema kwa upande wa barabara za mawe zimeongezeka kutoka kilomita 11.03 hadi kufikia kilomita 16.68 wakati kwa barabara za changarawe zimefikia kilomita 1,823.09 kutoka kilomita 1,252.
Mhandisi Mbanga anasema pia kumekuwepo na ongezeko la madaraja, makalvati, maboksi kalvati yaliyojengwa na TARURA Mkoa wa Mwanza ndani ya miaka mwili ya upngzo wa awamu ya sita.
Anasema madaraja yameongezeka kutoka madaraja 30 hadi kufikia madaraja 55, makalavati madogo yameongezeka kutoka makalavati 3,884 hadi kufikia 4,500, huku maboksi kalavati kutoka 208 hadi kufikia 338 wakati drifts zimeoengezeka kutoka 126 hadi kufikia 182.
“TARURA Mkoa wa Mwanza inapenda kumpongeza Mhe. Rais kwa kutimiza miaka miwili katika uongozi kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika miaka hiyo miwili ameboresha kwa kiasi kikubwa sekta ya miundombinu hususani ya barabara za wilaya kwa kuongeza bajeti ya utekelezaji wa miradi ya barabara kwa zaidi ya asilimia 100 na kuimarisha taasisi zenye jukumu la kusimamia miundombinu hiyo.
“Kero mbalimbali zinazohusiana na miundombinu ya barabara zimetatuliwa na zinaendelea kutatuliwa kutokana na ongezeko la bajeti. Tuna muahidi kutekeleza majukumu yetu kwa weledi na udailifu ili tuweze kutimia kauli mbiu yetu isemayo ‘Tunakufungulia barabara kufika kusiko fikika’,” anasema Mhandisi Mbanga.
Post A Comment: