Imeelezwa kuwa, Serikali ya Tanzania na Canada zimepanga kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali yakihusisha shughuli za utafiti wa madini, kujenga uwezo wa wataalamu na kushirikiana katika kuhamasisha shughuli za uwekezaji nchini ili kuvutia wawekezaji katika Sekta ya Madini.
Hayo yamebainishwa na Balozi wa Canada nchini Tanzania Kyle Nunas leo Mei 8, 2023 jijini Dar es Salaam alipokutana na kuzungumza na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali na Wataalamu kutoka Wizara na Taasisi katika kikao kilicholenga kuzungumzia shughuli za kuendeleza uchimbaji wa madini.
Balozi Nunas ameeleza kuwa, upo uwezekano mkubwa wa nchi ya Canada kushirikiana na Tanzania katika uendelezaji wa Madini ya Kimkakati yanayopatikana nchini ikiwemo kufanya utafiti ili kuiwezesha Tanzania kuzalisha madini hayo kwa wingi na uchimbaji wenye tija na endelevu.
“Madini ya kimkakati yanahitajika kwa wingi kwa sasa duniani kwa ajili ya kutumika katika teknolojia mbalimbali ikiwemo kutengeneza betri za magari ili kuzuia hewa chafu (clean energy), simu za mikononi, kompyuta na kutengeneza mota za magari yanayotumia umeme,” amesema balozi Nunas.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Mahimbali amesema kuwa, ushirikiano wa Tanzania na Canada katika Sekta ya Madini utaongeza tija kwenye uchumi, kuongeza ajira, kuwajengea uwezo watumishi ili kuwezesha watanzania kuzalisha madini hayo kwa wingi ikiwemo bidhaa zinazotokana na madini hayo.
“Tunaomba tuweze kuwa na ushirikiano na Canada katika kutangaza shughuli za uchimbaji madini zinazofanyika hapa nchini, tuendelee kukutana na kuzungumza mara kwa mara ili mchango wa Sekta ya Madini ukue katika uchumi wetu,” amesema Mahimbali.
Pia, Mahimbali amesema kuwa, Tanzania iko tayari kushirikiana na Cananda kuhakikisha Taifa linanufaika na rasilimali madini ikiwemo madini ya kimkakati ili kukuza uchumi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Dkt. Mussa Budeba amesema, ushirikiano wa Cananda kupitia taasisi (Geological Survey of Canada) na Tanzania katika utafiti wa kijiolojia ili kubaini upatikanaji wa madini muhimu na ya kimkakati katika maeneo ambayo hayajafanyiwa utafiti nchiini.
"Ni muhimu sana kubadilishana teknolojia mpya kutoka kwa wenzetu katika utafiti kwa kubadilishana wataalamu kupitia Makubaliano ya mashirikiano (MoU),” amesema Dkt. Budeba
Naye, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini Tume ya Madini Venance Kasiki amemueleza balozi Nunas maeneo ya kusaidia Tanzania katika Sekta ya Madini ni pamoja na kusaidia kujenga uwezo watumishi wa Wizara ya Madini kwenye Modeli za Fedha (Financial modeling) na uwezo huo utasaidia katika uchambuzi wa upembuzi yakinifu unaoletwa na wawekezaji kabla ya kutoa leseni za uchimbaji madini.
Tanzania imebarikiwa kuwa na madini mengi ya kimkakati yakihusisha madini ya nikeli, kinywe, rare earth elements, cobalt, chuma na madinini mengine ambayo ndiyo yanahitajika kwa sasa duniani kwa ajili ya kutumika katika teknolojia mbalimbali.
Post A Comment: