MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu Mei 5,2023, amefanya ziara katika Vijijiji vya Choda na Mkiwa vilivyopo jimboni humo kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo,kuzungumza na kusikiliza kero za wananchi kupitia mikutano ya hadhara.

Ziara ya Mtaturu ni muendelezo wa utaratibu aliojiwekea wa kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi ili kutoa fursa kwa wananchi kubainisha changamoto zao na yeye kwenda kuzisemea bungeni.

Akiwa katika ziara hiyo amekagua miradi kwenye shule ya sekondari Mkiwa ikiwemo ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na chumba kimoja cha maabara vyote vikiwa na thamani ya Sh.Milioni 90.

Akizungumza na wananchi Mtaturu amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan itaendelea kutoa fedha ili kutekeleza miradi kwenye sekta za Elimu,maji,Afya,miundombinu ya Maji,Umeme na barabara kama ilani ya uchaguzi inavyoelekeza.

Aidha,amesikiliza kero mbalimbali za wananchi zilizolenga hasa sekta ya ardhi ambapo wananchi wameeleza uwepo wa sintofahamu ya maeneo yao kutwaliwa bila wenyewe kushirikishwa na serikali ya Kijiji.

Katika mkutano huo wananchi walitaka kujua faida ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi na hasara zake na pia walitaka kujua faida za wawekezaji kwenye maeneo yao.

Baada ya kupokea maswali hayo Mbunge Mtaturu alimpa nafasi afisa ardhi wa wilaya ya Ikungi Ambrose Ngonyani ili atoe ufafanuzi wa kero na maswali waliyouliza wananchi.

Mzee Mathayo Dedu ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho amelalamikia eneo lake kutwaliwa bila ridhaa yake na mwekezaji.

“Mzee wangu nimepokea kilio chako nimuelekeze Mtendaji Kata kumuandikia Mkurugenzi wa halamashauri kero hizo zilizotolewa ili zipatiwe majibu ndani ya siku saba,”amesema Mtaturu.

Kupitia mkutano huo amewahimiza wananchi kutunza ardhi kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.

“Viongozi wa vijiji fanyeni mikutano ya kisheria ili kuwajulisha wananchi mipango ya serikali pamoja na kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua nah ii ndio dhana ya utawala bora,”amesisitiza.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wananchi,Diwani wa Kata ya Mkiwa Petro Mtiana amemshukuru Rais Samia kwa kuwapelekea fedha za miradi mingi katika kata yao ikiwemo Sh Milioni 310 za kutengeneza barabara za Mkiwa hadi Damaina na Mkiwa hadi Choda zilizokuwa kero sana hasa kipindi cha mvua.

“Nikushukuru pia mbunge wetu Mtaturu kwa kutuwakilisha vyema bungeni,umekuwa mdomo wetu wa kutusemea,na kupitia wewe umeomba fedha za miradi ambapo kupitia mfuko wa jimbo tumeletewa Sh Milioni 3.5 kwenye shule za msingi za Choda na Darajani,ahsante sana,”ameshukuru Diwani Mtiana.

        
Share To:

Post A Comment: