Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Fatma Taufiq akiongoza semina ya Wabunge iliyolenga kuwajengea uelewa juu ya masuala ya Watoto , Bajeti na masuala ya UKIMWI iliyofanyika ukumbi wa mikutano wa Dodoma Hoteli Jijini Dodoma Mei 14, 2023

 Imelezwa kuwa changamoto za mimba za utotoni katika jamii bado ipo kwa kuzingatia takwimu zilitolewa kutokana na matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.


Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Mhe. Fatma Taufiq wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ufunguzi wa semina kwa wabunge iliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya watoto na bajeti kwa kwa kuzingatia Matokeo ya sensa ya Watu na Makazi hususani kwa takwimu za watoto na namna ya kuendelea kupambana na masuala ya UKIMWI nchini.

Semina hiyo iliyofanyika Mei 14, 2023 Ukumbi wa Mikutano Dodoma Hoteli na kuhudhuriwa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Kamati ya Bajeti pamoja na Kamati ya Kuhumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI.

Mhe. Taufiq alieleza kuwa, kila mmoja anapaswa kuwa kinara katika kupinga mila na desturi zilizopitwa na wakati kwa kuendea kuwajengea uwezo watoto kujitambua na kukataa ndoa na mimba za utotoni.

“Watoto wajilinde na kujitunza wasijiingize katika ngono zembe, aidha suala la maadili, malezi na makuzi liwe letu wazazi na walezi kwa kutimiza wajibu na kuacha kuilaumu Serikali bila kusahau viongozi wa dini,”Alisisitiza Mhe.Taufiq.

Aliongezea kuwa, Kamati za Bunge zitaendelea kuishauri Serikali katika kutimiza majukumu yake ili kuifikia jamii kwa ujumla, na kuwa na Taifa lenye kizazi bora na salama na kuendelea kuwa na sauti za pamoja.

“Kamati za bunge na wabunge tutaendelea kuishauri Serikali katika masuala haya kwa kutoa kipaumbele katika mipango mbalimbali ya maendeleo hasa kipindi hiki ya bunge la bajeti, huku tukipinga vikali masuala ya mmomonyoko wa maadili kwa watoto wetu,”alisema

Akiongelea mafanikio ya semina hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Afya na UKIMIWI Mhe. Stanslaus Nyongo alieleza semina imewaongezea uelewa zaidi wa masuala ya watoto na namna ya kuendelea kuzungumza masuala yao katika nafasi walizonazo.

“Upo umuhimu wa kuwekeza kwenye human Capital kwa kuangalia watoto na kiasi gani tunato huduma kwa jamii hasa kwa kundi la watoto, hasa katika kuhakikisha watoto wanapata elimu kadiri inavyofaa,”alisema Mhe. Nyongo

Alifafanua kuwa, ipo haja ya jamii kuendelea kupinga ndoa za utotoni kwa kuzingatia athari zake kwa watoto.

“Ni wakati sasa kuendelea kupinga ndoa za utotoni na kuhakikisha mtoto analindwa, apewe elimu hasa ya masuala ya afya na uzazi ili kuwajengea uelewa wa kuweza kuchanganua mambo mazuri na mabaya na kuweza kujilinda kwa kizazi hiki na kile cha badae,”alisisitiza Mhe Nyongo

Naye Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) Bi. Scholastica Williams alipongeza jitihada za Serikali katika kupambana na unyanyapaa katika jamii huku akitoa wito wa kuendelea kupinga vitendo hivyo.

“Tupinge unyanyapaa kwa jamii, tuhamasishe WAVIU kuendelea kutumia dawa ili kuwa na uelewa wa pamoja katika mapambano haya,”alisema

Aidha alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi na walezi kuwa wazi kwa watoto wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI nchini kwa kuendelea kuwashauri, kuwapa elimu ya matumizi sahihi ya dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI ili kuwa na jamii salama.

“Jamii isaidie na kuendelea kuwa wawazi kwa watoto kuhusu UKIMWI, maana kumukuwa na dhana potofu ya kuficha masuala haya na kuyaonea aibu hasa matumizi ya dawa za ARV hali ambayo si sahihi, wazazi wawaeleze ukweli watoto wao ili waendelee kuzingatia matumizi na waelewe kuwa, kupata Maambukizi si mwisho wa maisha,”alisema Scholastica.

Mtaalamu wa Mawasiliano kutoka UNICEF Bi. Usia Nkhoma Ledama akiwasilisha mada ya hali ya watoto na ujumbe maalum wakati wa semina hiyo iliyofanyika Dodoma Hotel.



Baadhi ya washiriki wa semina hiyo wakifuatulia mawasiliasho wakati wa semina hiyo.

Naibu Afisa Mtendaji Mkuu Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) Bi. Scholastica Williams akizungumza wakati wa semina hiyo.
Share To:

Post A Comment: