Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh.Anthony Mavunde ameiomba serikali kuipandisha hadhi Hospital ya Benjamin Mkapa kuwa Hospitali ya Taifa na kuongeza madaktari bingwa bobezi ili kuimarisha huduma ya afya kwa wakazi wa Mkoa wa Dodoma na mikoa jirani ambao wanahudumiwa na Hospitali hiyo.
Mavunde ameyasema hayo jana katika Hospitali ya Benjamini Mkapa mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim M. Majaliwa wakati wa uzinduzi wa huduma ya upandikizaji wa Uloto(Bone marrow) kwa watu wenye seli mundu(sickle cell).
“Ninaishukuru sana serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mh Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za afya Jijini Dodoma,uwepo wa hospitali ya Benjamin Mkapa umesaidia kusogeza huduma muhimu za matibabu kwa wanadodoma ambao zamani walikuwa wanazifuata huduma hizi hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Ombi langu kwasasa ni hospitali hii kupewa hadhi ya Taifa na kuongezewa madaktari bingwa bobezi ili iweze kuwahudumia watanzania wengi zaidi kutokea Dodoma na mikoa ya jirani.”Alisema Mavunde
Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri Mkuu Mh Kassim M. Majaliwa amesema Serikali iliamua kuwekeza shilingi bilioni 2.7 ili kuanzisha huduma ya upandikizaji uloto na kupunguza gharama za matibabu hayo kwa wananchi na kutumia fursa hiyo kumtaka Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu kuangalia uwezekano wa kuongeza madaktari bingwa bobezi katika hospitali ili kufikisha huduma kwa urahisi kwa wananchi.
Naye Waziri Ummy Mwalimu amesema wizara hiyo inaangalia uwezekano wa kuipandisha hadhi hospitali hiyo ili iwe hospitali ya Taifa badala ya kuendelea kubakia kuwa ya kanda kwamba kwa sasa wameanza kujenga kituo cha kutoa tiba ya kansa na pia kujenga kituo cha umahiri cha matibabu ya moyo ili kuimarisha utoaji wa huduma kwenye hospitali hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika alimueleza Waziri Mkuu kwamba tangu Januari 19, mwaka huu hadi leo, wamefanikiwa kupandikiza uloto kwa watoto watatu na wote wanaendelea vizuri. Watoto wawili wanatoka kijiji jirani cha Mapinduzi na mmoja anatoka eneo la Area D hapahapa Dodoma.
Alisema kufanyika kwa upandikizaji wa uloto kwenye hospitali hiyo, kumeifanya Tanzania iwe miongoni mwa nchi saba zinazotoa huduma hiyo barani Afrika. Alizitaja nchi nyingine zinazotoa huduma hiyo kuwa ni Algeria, Afrika ya Kusini, Misri, Morocco, Nigeria na Tunisia. “Kwa mantiki hiyo, Tanzania inakuwa nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuanza kutoa huduma hiyo.
Post A Comment: