Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo May 17, 2023 wakati akitoa taarifa ya maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani ambayo yataanza kuadhimishwa mkoani hapa kesho May 18, 2023 na kilele chake itakuwa May 21, 2023 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa ni Makamu wa Rais Dkt. Phillip Isdor Mpango. 

                                             .......................................................................

Na Dotto Mwaibale, Sinida

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Phillip Isdor Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya siku ya nyuki duniani kwa mwaka 2023 ambayo yatafanyika May 21, 2023 mkoani Singida katika viwanja vya Bombadia. 

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba wakati akitoa taarifa ya maadhimisho hayo kwa waandishi wa habari ambapo alisema yatakuwa kwa muda wa siku nne kuanzia kesho May 18, 2023 hadisiku ya kilele chakeMay 21, 2023 chini ya Kauli mbiu isemayo  "Tuwalinde Nyuki kwa Ustawi wa Mazingira na Usalama wa Chakula" 

“Leo nimewaalika hapa kwa lengo moja kuu nalo ni kuzungumzia maadhimisho ya siku ya nyuki duniani kitaifa kwa mwaka huu wa 2023. Maadhimisho haya ni utekelezaji wa azimio la Baraza la Umoja wa Mataifa la Disemba 20, 2017 ambalo lililenga kutambua mchango wa mdudu nyuki katika usalama wa chakula na uhifadhi wa mazingira,” alisema Serukamba.

Serukamba alisema maadhimisho hayo yatajumuisha matukio mbalimbali kama, maonesho ya bidhaa na huduma za ufugaji nyuki ambapo wadau wataweza kufahamu faida za mazao zaidi ya sita yanayopatikana kutoka kwa mdudu nyuki na kampeni ya utundikaji mizinga itakayofanyika Wilaya ya Itigi katika Kijiji cha Kitaraka kwa lengo la kuwajengea wananchi uelewa kuhusu mbinu bora za ufugaji nyuki.

Alitaja mambo mengine yatakayofanyika ni safari maalumu zilizo andaliwa kwa lengo la kuweza kutembelea vivutio vilivyopo katika mkoa wetu wa Singida safari zilizopewa jina la ’Nyuki Safari’ na semina zitakazo husisha elimu ya mambo muhimu katika ufugaji nyuki mfano namna ya kuongeza ubora wa mazao ya nyuki na mwisho ni tukio la sherehe za kilele zitakazofanyika May 21, 2023.

Serukamba alisema maadhimsho ya siku ya nyuki duniani kufanyika mkoani Singida ni fursa kwa wadau kuweza kujifunza pamoja na mambo mengine mbinu za kuweza kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki pia, kuweza kupata masoko ya mazao ya nyuki. kama inavyofahamika kuwa Mkoa wa Singida umekuwa ukifanya shughuli za ufugaji nyuki kwa kipindi kirefu na kuweza kuchangia kipato cha wananchi wa mkoa huo na kuwa wakulima wakubwa wa zao la alizeti nchini wakiwepo na wa Mkoa wa Singida wameendelea kunufaika na huduma ya uchavushaji kutoka kwa mdudu nyuki.

Serukamba alitumia nafasihiyo kutoa rai na kuwakalibisha wananchi wote wa Mkoa wa Singida na mikoa jirani kuweza kushiriki katika maadhimisho hayo ambayo ni muhimu.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Ufugaji Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Daniel Pancras, akizungumzia umuhimu wa maadhimisho hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbas alisema yamelenga kutambua umuhimu wa mdudu nyuki katika uhifadhi wa mazingira na usalama wa chakula.

Alisema mdudu nyuki ni muhimu sana kwani ni miongoni mwa wadudu wachavushaji waliopo duniani na uchavusha takribani asilimia 80 ya mazao yote ya chakula hivyo basi umuhimu wake si katika kuzalisha asali tu bali na katika utunzaji wa mazingira.

”Mazingira mazuri tunayoyaona,ikiwemo miti, mimea mbalimbali tunayoiona ikiwa imestawi vizuri na kustawi kwake kuna changiwa kwa kiwango kikubwa na uwepo wa  mdudu nyuki,” alisema Pancras.

Pancras alisema tukiwa kama sehemu ya watu duniani kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha anatunza mazingira ya mdudu nyuki na mazalia yake na kufurahia uwepo wake kutokana na faida tunazozipata ikiwemo usalama wa chakula.

Alisema katika maonesho hayo kutakuwa na bidhaa za aina tofauti tofauti kutoka kwa  wadau mbalimbali  ambao watazionesha pamoja na teknolojia za ufugaji wa nyuki na utunzaji wa mazingira na pia kutakuwa na semina ambazo zimejikita kuangalia mchango wa mdudu nyuki katika uchavushaji na madhara yanayo tokea dhidi ya mdudu huyo baada ya kutumia viuatilifu kwa njia ambayo sio sahihi na kuweza kuwaaathiri wadudu wachavushaji wakiwemo nyuki.

Aidha, Pancras alisema kutakuwa na uangaliaji wa ubora wa mazao ya nyuki na miongozo mbalimbali inayosimamia sekta ya nyuki na kuwa jambo kubwa ni ile Siku ya Safari za Nyuki ambayo itatumika kutangaza na kuhamasisha utalii wa Mkoa Singida.

Alisema Nyuki Safari ni zao jipya ambao ni utalii wa nyuki ambapo wananchi wote na wadau watakao kuwepo kwenye maadhimisho hayo wataweza kwenda kutembelea maeneo zinapofanyika shughuli za nyuki na kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Mkoa wa Singida na kuwa jambo hilo linakwenda kufungua hamasa ya watu kwenda  kuwekeza katika nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya utalii na kuwa lengo la wizara hiyo kushirikiana na mkoa katika maadhimisho hayo lilikuwa ni kuufanya mkoa huo ukue kiuchumi  wakizingatia kuwa upo jirani na makao makuu ya nchi Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Maendeleo ya Ufugaji Nyuki, Wizara ya Maliasili na Utalii, Daniel Pancras, akizungumzia umuhimu wa maadhimisho hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbas.

Ufugaji bora wa nyuki unavyofanyika.
Muuonekano wa mdudu nyuki.
Bidhaa za nyuki zikiwa sokoni.
Muonekano wa mzinga wa nyuki wa kisasa. 
Muonekano wa mabanda ya maonesho ya maadhimisho hayo katika viwanja vya Bombadia vilivyopo Manispaa ya Singida wakati wa maandalizi yake.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: