Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa madaktari na watoa huduma wote kuendelea kufanya kazi kwa kujituma, upendo , kujitoa na kuzingatia weledi na maadili ya tasnia ya utabibu ili kuokoa maisha ya Watanzania.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Ufunguzi wa Jengo la Huduma za Dharura (EMD) katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Meru mkoani Arusha leo tarehe 18 Mei 2023. Amesema viongozi wa hospitali hiyo wanapaswa kutoa umuhimu mkubwa katika kutunza vifaa tiba kwa kuhakikisha vinafanyiwa ukarabati kwa wakati ili vidumu kwa muda mrefu. Aidha ameongeza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya afya ili kuhakikisha watanzania kote nchini wanapata huduma bora za afya na kwa ukaribu zaidi.
Amesema serikali inatarajia kukabidhi magari mawili ya wagonjwa katika hospitali hiyo pamoja na madaktari zaidi ya 25 kwa Wilaya ya Arumeru ikiwa ni njia ya kukabiliana na changamoto za upungufu wa rasilimali watu katika sekta ya afya wilayani humo.
Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali za mara kwa mara zinazogharimu maisha ya wananchi. Amesema asilimia kubwa ya wagonjwa wanaofikishwa katika huduma za dharura wanatokana na ajali hivyo amelisihi jeshi la polisi kusimamia sheria zilizowekwa kikamilifu ili kuendelea kupunguza adha ya ajali nchini.
Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa wananchi wa Arumeru kuhakikisha wanatatua migogoro kwa njia ya amani na upendo na kuacha kujichukulia sheria mkononi ambazo husababisha madhara katika jamii kama vile majeruhi na vifo. Vilevile amewasihi wajawazito kuona umuhimu wa kuhudhuria kliniki kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili kuepukana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kujifungua.
Pia Dkt. Mpango ametoa wito kwa Wakala ya Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kutoa kipaumbele kwa ukarabati wa barabara zilizopo katika halmashauri ya Wilaya ya Meru ili ziweze kuwasaidia idadi kubwa ya wakulima waliopo katika halmashauri hiyo kuyafikia masoko kirahisi.
Ameongeza kwamba Serikali itaendelea kuboresha huduma za jamii katika mkoa wa Arusha na kuutambua mkoa huo kama eneo la kimakakati kwa sekta ya utalii hapa nchini. Amewaasa wananchi wa mkoa huo kuendelea kudumisha amani na kuwa wakarimu kwa wageni mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ili kuchochea utalii.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela ameishukuru serikali kwa ujenzi wa huduma za jamii katika mkoa huo ikiwemo huduma za afya. Amesema Wilaya ya Arumeru ni Wilaya kiongozi kwa uzalishaji wa chakula katika mkoa wa Arusha lakini inakabiliwa na changamoto za huduma za maji na miundombinu ikiwemo barabara kutokana na kuzungukwa na milima.
Mongela ameongeza kwamba uongozi wa mkoa utaendelea kusimamia kikamilifu fedha za miradi za miradi zinazopelekwa mkoani humo ili thamani ya miradi iweze kuonekana.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru Dkt. Maneno Focus amesema mradi huo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi kutokana na mpangilio mzuri wa vyumba vya huduma na uwepo wa vifaa tiba vya kisasa. Ameongeza kwamba jengo la huduma za dharura litaweza kunufaisha wananchi zaidi ya laki 3.3 wa halmashauri ya Wilaya ya Meru pamoja na kuwa msaada kwa wahanga wa ajali zinazotokea karibu na eneo hilo.
Mradi wa ujenzi wa Jengo la Huduma za Dharura katika hospitali ya Halmashauri ya Wilaya Meru umegharimu shilingi milioni 809 ambapo ujenzi wa jengo ni shilingi milioni 330 na gharama za vifaa tiba ni shilingi milioni 476.
Post A Comment: