KAMISHINA wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mabula Nyanda amesema mwelekeo wa Wizara ya Maliasili na Utalii ni kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa kwa nguvu zote ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vya Utalii vilivyopo katika maeneo yote yanayosimamiwa kisheria


Ameyasema hayo Mei 11, 2023 alipokuwa akizungumza na Wahifadhi wa Pori la Akiba Muhesi lililopo Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida katika siku ya pili ya ziara yake Kanda ya kati."Kubwa lililotuleta hapa, ni kutoa mwelekeo wa Wizara ya Maliasili na Utalii kufuatia mabadiliko ya uongozi wa juu" amesema

"Kwa sasa mwelekeo wa uongozi wa juu wa Wizara, kwanza kabisa wanataka tuhakikishe kwamba maeneo na rasilimali iliyopo katika maeneo tunayosimamia inakuwa salama, tuilinde Kwa nguvu zote" amesisitiza Kamishna Mabula

Kamishna huyo amesema ili waweze kuzilinda vyema rasilimali hizo, Wahifadhi Wote wa TAWA hususan wa Pori la Akiba Muhesi wanapaswa kwanza kuzifahamu vyema rasilimali walizonazo, kujua mahali zilipo na kuzitambua hivyo ameelekeza Wahifadhi Wote Kwa kutumia GPS na teknolojia nyingine kuhakikisha wanazitambua rasilimali zilizopo katika maeneo yao.

Sambamba na hilo amesema Wahifadhi wanalojukumu la kubuni na kuibua mazao mapya ya Utalii na kuhakikisha wanayatangaza Kwa Kasi kubwa Ili kuongeza idadi ya watalii na hivyo kuongeza mapato Serikalini.

Pia Kamishna Mabula amesema ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za Uhifadhi ni jambo linalopewa kipaumbele sana na uongozi wa Wizara Kwa sababu hiyo ameelekeza uongozi wa Pori la Akiba Muhesi kushirikiana Kwa karibu na Serikali za vijiji, kata na wilaya Ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kiuhifadhi ikizingatiwa kuwa Pori hilo limezingukwa na takribani vijiji 23.

Mbali na kutoa mwelekeo wa Wizara, Kamishna Mabula amesema ziara yake pia imelenga kusikiliza maoni chanya ya wahifadhi yanayolenga kuiimarisha na kuipeleka mbele TAWA ikiwa ni pamoja na kujua changamoto wanazopitia katika Pori hilo.

Awali akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Pori, Kamanda wa Pori la Akiba Muhesi C II Paul Lunimba amesema Wadau wa Uhifadhi (TFS, WCS na STEP) wamekuwa na mchango mkubwa katika shughuli mbalimbali za Uhifadhi na wanatoa ushirikiano mkubwa kwa uongozi wa Pori hilo hasa katika doria na kutoa elimu kuhusu Wanyamapori Wakali na Waharibifu kiasi Cha kupelekea idadi ya Wanyamapori kuongezeka Kwa wingi katika hifadhi hiyo

Amesema changamoto kubwa ni suala la wanyamapori wakali na waharibifu ambao huwasumbua wananchi katika vijiji jirani na pori hilo, na hiyo ni kutokana na uchache wa watumishi na vitendea kazi jambo ambalo limemlazimu Kamishna Mabula kutolea majibu ya haraka na kuahidi Menejimenti ya TAWA kupeleka vifaa maalumu vya kisasa vya kudhibiti Wanyama Tembo haraka iwezekanavyo kurejesha amani kwa wakazi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.

Aidha kwa niaba ya watumishi ameipongeza Menejimenti ya TAWA Kwa kuboresha maisha ya watumishi kimaslahi hali ambayo imepelekea morali ya watumishi hao kuongezeka na kufanya kazi Kwa kujituma bila kujali Changamoto zinazowazunguka.







Share To:

Post A Comment: