NA DENIS CHAMBI, TANGA.
KAMANDA wa jeshi la Polisi mkoa wa Tanga Henry Mwaibambe amewaonya madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda kutokujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wanapohitaji dhamana baada ya kukamatwa huku akiwaonya wenyeviti wa mitaa kutokuwatetea wahalifu wanapokamatwa na jeshi hilo kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo ya uhalifu.
Ametoa rai hiyo may 25, 2023 wakati alipofanya kikao cha pamoja na viongozi wa serikali za mitaa pamoja na Madereva wa pikipiki (Bodaboda) ,Bajaji kikijumuisha pia viongozi wao ikiwa ni makakati wa pamoja wa kupunguza ajali za barabarani na matukio ya kiuhalifu huku akiwataka madereva hao kutokupakia abiria zaidi ya mmoja kwenye vyombo vyao hususani wanafunzi ili kuondokana na adha ambazo wanaweza kukumbana nazo.
"Suala la dhamana kwenye kituo cha Police nendeni mkamuone mkuu wa kituo mwenyewe au mkuu wa upelelezi wala sio mtu mwingine nasema haya kwasababu ili kama kuna Askari ameomba rushwa tujue hatutaki mtu yeyote wa katikati na wala hairuhusiwi Askari yeyote kumuomba rushwa au wewe utoe rushwa ili upate dhamana hatutaki tabia ya namna hii" alisema Kamanda Mwaibambe.
Aidha amewataka madereva wote wa pikipiki kutii sheria za barabarani ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakuwa na leseni pindi wanapotumia vyombo vya usafiri huku akiwataka kutoa ushirikiano na taarifa kwa jeshi hilo pale wanapoona wahalifu katika maeneo yao.
"Niwaombe sana bodaboda mtii sheria za barabarani nataka tuanze ukurasa mpya sasa hamuwezi kutushinda tunataka mfanye kazi lakini msivunje sheria nawaomba Sana epukeni pia kuwapa watu bodaboda zenu wengi wanatoa namba na wanakwenda kufanyia uhalifu zipo pikipiki nyingi tumezikamata kwa uhalifu, nyie mnayo nafasi ya kujua wenzenu ambao sio wazuri" alisema kamanda
Pamoja na hayo kamanda Mwaibambe alisema jeshi hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupambana na kukomesha wizi wa simu ambao ulikuwa umeshamiri ndani ya mkoa wa Tanga ambapo kwa sasa wamefikia asilimia 90 kudhibiti aina hiyo ya uhalifu.
Akizungumza katibu wa umoja wa waendesha pikipiki na bajaji jiji la Tanga 'UWAPIBATA' Juma Mganga alisema kuwa katika kutatua changamoto ya uhalifu kwa upande wao wameanzisha mfumo rasmi wa kuwatambua bodaboda wote waliopo ndani ya jiji la Tanga ambapo wamekuja na fomu maalumu ya usajili kwa kila mtu anayefanya kazi hiyo ili inapotokea changamoto yeyote inayomhusu iwe ni rahisi kuweza kupata msaada wa haraka.
"Sisi viongozi wa bodaboda tumeanzisha mfumo usajili tuna fomu kwaajili ya kumtambua bodaboda wetu ambapo fomu ile itaanzia kwenye ofisi ya serikali ya mtaa wataigonga muhuri na sisi ofisi ya bodaboda tayari tuna file na tutaiweka ambayo inatujulisha kwamba huyu bodaboda anapatikana kituo fulani, lakini wakati tunapotaka kuwasajili hawa bodaboda wetu kuna baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa hawatupi ushirikiano mzuri naamini tukishirikiana vizuri hata uhalifu wa mtaani utaisha" alisema Mganga.
Akizungumzia tabia ya baadhi ya madereva wa bodaboda kupenda kupakia abiria zaidi ya mmoja hususani wanafunzi jambo ambalo linaweza kuchangia ajali za barabarani Mganga alisema kuwa wamejipanga kwa kushirikiana na wazazi, walezi kukomesha tabia hiyo.
"Ili tutatue vizuri changamoto hii bodaboda wetu wabebe abiria sahihi wazazi nao washirikishwe kwasababu wazazi nao ni tatizo wengi wanaweza kuwalazimisha bodaboda kupakia watoto zaidi ya mmoja na tunaamini wenyeviti hawa watatufikishia ujumbe sahihi kwa wazazi waliopo majumbani na upande wa bodaboda kwenye ubebaji lazima tushirikiane kwenye hili" aliongeza
Kwa upande wake mwenyekiti wa wenyeviti wa mitaa ya jiji la Tanga Buno Omari amewaomba bodaboda kutokujichukulia sheria mkononi pale mmoja wao anapopata changamoto ikiwemo ya uhalifu badala yake washirikiane vyema na viongozi wa serikali za mitaa ili sheria ziweze kufwata mkondo wake.
"Bodaboda wengi wana matatizo ya kujichukulia sheria mkononi sasa wanapokuja kwenye serikali za mitaa wanakumbana na wenyeviti lazima wakupe ushirikiano wa hali na mali wa kumkamata huyo mhusika lakini wanapokuwa bodaboda wanajikusanya kuja mtaani kufanya vurugu hiyo lazima watakutana na vikwazo vya wenyeviti nawaomba umoja wa bodaboda wakae vizuri na wenyeviti wa mitaa walitatue hili tatizo" alisema Omari.
Kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Tanga Henry Mwaibambe (katikati) waliokaa akiwa pamoja na viongozi wa umoja wawaendesha pikipiki na bajaji mkoa wa Tanga 'UWAPIBATA' wa kwanza Kulia waliokaa Ni mwenyekiti wa wenyeviti wa mitaa jiji la Tanga Buno Omari wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kikao hicho. Picha zote na Denis Chambi.
Baadhi ya wenyeviti wa mitaa na waendesha bodaboda wa jiji la Tanga
wakiwa kwenye kikao cha pamoja kilichoitishwa na kamanda wa jeshi la
Polisi mkoa wa Tanga Henry Mwaibambe kujadili kuhusu kuimarisha ulinzi
na usalama ikiwemo kufwata sheria za barabarani.
Kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Tanga Henry Mwaibambe akizungumza na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda pamoja wenyeviti wa mitaa ya jiji la Tanga wakati walipokutana may 25 katika kikao cha pamoja kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama na usalama barabarani, kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa jeshi hilo 'Police Officers Mess'
Post A Comment: