Na John Walter-Manyara
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa Mheshimiwa Dogo Iddy Mabrouk amesema hatochoka kuwaasa vijana mpaka wabadili mienendo mibaya waliyonayo.
Amezungumza hayo akitoa semina ya maadili kwa Wanafunzi wa chuo Cha Ualimu Mamire pamoja na Wazazi ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya wiki ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Amesema vijana wengi wamekuwa wakiharibu tamaduni za nchi ya Tanzania kwa kuiga vitendo visivyofaa kutoka mataifa mengine kupitia mitandao mbalimbali na kwenye Runinga.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Babati Vijijini Filbert Mdaki amesema mwanamke anahitaji kudekezwa na kupendwa na sio kupigwa au kunyanyaswa kwa namna yoyote.
Amesema ni wazi kwa sasa kumekuwepo na changamoto ya mmomonyoko wa maadili ikiwemo ndoa za jinsia moja ambapo wazazi, walezi na jamii kwa ujumla inapaswa kukemea vikali ili kuondokana na taifa lisilofaa kwa vizazi vya sasa na baadaye.
Amewataka wanafunzi kuanzia ngazi ya msingi hadi vyuo kufuata mila na desturi za Tanzania na kuacha kuiga za watu ili kutimiza malengo yao na taifa kwa ujumla.
Wiki ya wazazi mwaka 2023 iliyozinduliwa Mei 6 katika kata ya Galapo wilaya ya Babati mkoani Manyara ambayo itahitimishwa mei 9,2023 mjini Babati, inaongozwa na Kauli mbiu isemayo "Taifa bora,hutokana na malezi bora ya watoto".
Post A Comment: