Na Benny Mwaipaja, WFM, Arusha

 

Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu lameck Nchemba, amezishauri nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya utafiti ili kufahamu sababu za nchi hizo kushindwa kufikia vigezo mtangamano wa uchumi mpana ambavyo ni moja kati ya vigezo vya nchi hizo kufanikisha itifaki ya Umoja wa Sarafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ifikapo mwaka 2031.

 

Dkt. Nchemba alitoa rai hiyo wakati wa mkutano wa 15 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Fedha na Uchumi la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Jijini Arusha ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulipokea na kujadili taarifa mbalimbali za mkutano uliopita wa Baraza hilo.

 

Miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ni pamoja na mashauriano ya kibajeti  kwa mwaka wa fedha 2023/2024, taarifa ya Mkutano wa 26 wa Kamati ya Magavana wa Benki Kuu za Jumuiya hiyo; Mwenendo wa hali ya uchumi na maendeleo ulimwenguni pamoja na hatua zilizofikiwa na nchi wanachama katika kukidhi vigezo vya mtangamano wa uchumi mpana wa Jumuiya hiyo. 

 

Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania imekidhi vigezo vyote vya mtangamano wa uchumi mpana isipokuwa kigezo cha nakisi ya bajeti kinachopaswa kuwa chini ya asilimia 3. Kwa upanda wa Tanzania kigezo hicho kimefikiwa kwa asilimia 3.3 wakati nchi zote za Jumuiya hiyo zikishindwa pia kufikia kiwango kinachotakiwa ili kuwezesha kufikiwa kwa Umoja wa Fedha unaolenga kuwa na sarafu moja.

 

“Tathmini inaonesha kuwa nchi wanachama hazikuweza kufikia vigezo vyote vya msingi vya mtangamano wa kiuchumi kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo UVIKO-19 na ongezeko la mahitaji ya rasilimali fedha kwa nchi wanachama katika kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu muhimu kwa jamii” alisema Dkt. Nchemba

 

Alishauri Baraza la Mawaziri wa Fedha na Uchumi kuielekeza Sekretarieti ya Jumuiya hiyo kufanya utafiti kuhusu kukwama kwa nchi zote za Jumuiya hiyo kufikia kigezo hicho na kuchambua na kuandaa mwongozo wa sera utakaoziwezesha nchi wanachama kutatua kikwazo hicho.

 

Suala la nchi wanachama kufikia vigezo vya mtangamano wa uchumi mpana ni muhimu katika kufanikisha itifaki ya Umoja wa Sarafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

 

“Baadhi ya nchi wanachama zimekuwa hazifikii malengo katika kufikia vigezo hivi na kumekuwa hakuna hatua zinazochukuliwa ili kuhakikisha nchi zote wanachama zinafikia vigezo  kabla ya kuwa na sarafu moja ifikapo 2031, kwa sababu vigezo vya kupima suala hilo vimebadilika kwa kiwango kikubwa ikiwemo kuongezeka kwa misaada, ruzuku na mikopo kwa nchi za wanachama” alisema Dkt. Nchemba

 

Mapendekezo hayo ya Mheshimiwa Dkt. Nchemba yameungwa mkono na Mawaziri wa Fedha na Uchumi wa Kenya, Rwanda, na Burundi, pamoja na wawakilishi wa Mawaziri wa Fedha wa Sudan Kusini na Uganda, ambapo wamesema kuwa kutokana na vigezo hivyo kuwekwa muda mrefu na kushindwa kufikiwa kuna maanisha kuwa kuna haja ya kuviangalia upya.

 

Aidha, Dkt. Nchemba, aliwaalika Mawaziri hao wa Fedha na Uchumi wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kuwashawishi Wakuu wao wa nchi, kushiriki Mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika wa masuala ya maendeleo ya rasilimali watu (Africa Heads of State Human Capital Development Summit) utakaofanyika Dar es Salaam mwezi Julai, 2023

 

Katika Hatua nyingine, Baraza la Mawaziri hao wa Fedha na Uchumi wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana kusoma Bajeti Kuu za Serikali hizo tarehe 15 Juni, 2023, ambapo kaulimbiu ya Jumuiya itakuwa “kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, kuhimili na kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha sera za uzalishaji ili kuboresha hali ya maisha”.

Share To:

Post A Comment: