Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Watanzania kutumia kwa usahihi barabara zinazojengwa kwa kuondokana na mwendokasi na kutozingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazojitokeza.
Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Barabara ya kiwango cha lami ya Mianzini – Ngaramtoni Juu yenye urefu wa kilometa 18 akiwa ziarani mkoani Arusha leo tarehe 18 Mei 2023. Amesema taifa linaendelea kupoteza nguvukazi kwa vifo na ulemavu wa kudumu kutokana na matukio ya ajali za barabarani.
Amewasihi madereva wa vyombo vya moto kuwa waangalifu,watumiaji wa bodaboda kuzingatia kofia ngumu pamoja na abiria kuvaa mikanda wawapo safarini. Pia amewahimiza Askari wa Usalama barabarani kusimamia sheria kikamilifu pasipo kuwaonea wananchi na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Halikadhalika Makamu wa Rais amemuagiza mkandarasi anayejenga barabara ya Mianzini – Ngaramtoni Juu kutoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi wa mkoa wa Arusha ili waweze kunufaika na mradi huo muhimu.
Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita imeonesha nia ya dhati na vitendo katika kuboresha miundombinu hususani maeneo ya vijijini ambapo tangu kuingia madarakani imeongeza bajeti ya TARURA kutoka bilioni 275 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia bilioni 818.02 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 utakaoanza mwezi julai. Ameongeza kwamba lengo ni kuhakikisha barabara za vijijini zinapitika vema na kwa urahisi ili kuchochea shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa barabara hiyo unalenga kufungua upya miundombinu katika Wilaya ya Arumeru na kuwapa unafuu zaidi wananchi kuyafikia masoko katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa gharama nafuu na muda mfupi zaidi.
Pia amesema barabara hiyo itatumika kama barabara ya mchepuko (bypass) ili kupunguza msongamano katikati ya jiji la Arusha.
Ujenzi wa barabara ya Mianzini – Ngaramtoni Juu kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 18 inagharimu shilingi bilioni 22.2.
Post A Comment: