Bertha Mollel, Arusha.
Makamu wa Rais , Dkt Philip Mpango ameziagiza taasisi zote zinazotoa huduma za kifedha nchini kupunguza zaidi kiwango cha riba na masharti ya mikopo ili kusaidia makundi ya chini kunufaika.
Dkt. Mpango ametoa agizo hilo leo May 19 jijini Arusha wakati akifungua mkutano kwa wanahisa wa benki ya CRDB unaofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Aicc.
Dkt. Mpango amesema kuwa makundi ya mbalimbali ya wachimbaji wadogo wa madini,wavuvi, wakulima na wafugaji wamekuwa waoga kujiingiza kwenye mikopo hii kutokana na riba kuwa inayotozwa na taasisi za fedha nchini ni ambayo ni zaidi ya asilimi tisa.
"Taasisi nyingi za fedha zimekuwa zikitoa mikopo ya riba kwa asilimia 9 na zaidi hivyo naomba muone jinsi gani mnaweza kupunguza zaidi ili kuwapa fursa wafanyabiashara wadogo na wananchi waliopo vijijini kuweza kupata huduma zenu ili nao wapige hatua kiuchumi"
Dkt. Mpango pia aliwataka taasisi hizo kufungua matawi zaidi maeneo ya vijijini ili kutatua changamoto ya ukosefu wa huduma za kibenki huko akidai kuwa ni asilimia nane pekee ndio wanapata huduma.
"Pia nitoe pia wito kwenu kuzingatia ufanisi katika utendaji kazi ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji kwa kutumia Tehama , lakini kuhakikisha hakuna mikopo chechefu mipya na kuzingatia ukomo wa asilimia 5 uliowekwa na benki kuu ya BOT" alisema.
Zaidi Dkt. Mpango aliwapongeza benki ya CRDB kwa kwa kuwa mdau mkubwa katika kusapoti shughuli mbali mbali za serikali kupitia kampeni zao ikiwemo ya pendezesha Tanzania inayohusika na upandaji wa miti nchi nzima.
Mwenyekiti wa bodi ya benki ya CRDB, Dkt Ally Laay ameomba serikali kupitia wizara ya elimu kuandaa mitaala maalumu ya kuwafundisha wanafunzi umuhimu wa kuwekeza katika Hisa ili kuwapa elimu ya fedha wakiwa na umri mdogo.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuwekeza kwenye hisa kwani Hadi sasa Taifa lina mwako mdogo sana ya uwekezaji katika maswala ya Hisa
"Bado kuna ufahamu mdogo kwa jamii katika maswala ya Hisa na uwekezaji wa fedha , pendekezo letu ni kuwa tuna haja ya kufundisha somo la mitaala kwenye shule zetu ili vijana wapate ufahamu wakiwa wadogo jambo ambalo litaleta fikra chanya katika uwekezaji wa maswala ya Hisa."amesema.
Awali Mkurugenzi wa benki ya CRDB, Abdulmajjid Nsekela alisema kuwa utaratibu waliojiwekea wa kila mwaka kutoa semina kwa wanahisa umeongeza hamasa kwa wananchi kununua hisa katika Benki hiyo.
Alisema idadi ya wanahisa hapa nchini waliojiunga na mabenki ni chache kwa mabenki mbalimbali kutokana na kutokuwa na elimu ya fedha ndio maana kumekuwa na utaratibu wa kutumia semina ya wanahisa.
"Watanzania tupo zaidi ya milioni 60 lakini ukiangalia kwenye mabenki yote nchini wateja hawazidi milioni 10 wenye akaunti na hiyo ni kutokana na elimu ndogo ya fedha ndio maana benki hii imeamua kufanya maboresho ya kuwa na semina ya wanahisa jambo lililosaidia kuongeza idadi ya wateja wa benki hiyo" alisema.
Alisema wanahisa wa Benki hiyo wanatarajia kunufaika na gawio nono la asilimia 45 kwa kila hisa tofauti na mwaka jana lilikuwa ni asilimia 35 na hiyo ni baada ya Benki hiyo kupata faida ya shilingi 365bilioni baada ya Kodi.
Post A Comment: