Makamu wa Rais, Mhe. Philipo Isdor Mpango ameipongeza  Wizara  ya Maliasili na Utalii  kwa kuanza kufanya vizuri  kwenye sekta ya utalii  hivi karibuni  kutokana na mikakati iliyojiwekea  hususan baada ya kumalizika kwa ugonjwa wa uviko 19 huku akiwataka watendaji kusimamia  makusanyo  yanayopatikana na  kuendelea kuwa wabunifu ili  kupita malengo waliojiwekea.

Pia ametoa wito kwa Wizara  kumwandalia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan Tuzo maalum kwa  kutambua mchango wake wa maendeleo katika nchi na kufufua sekta ya utalii nchini.


Kauli hizo amezitoa leo Mei 16, 2023 Karatu mkoani Arusha wakati akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa ofisi ya Makao makuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kwenye ufunguzi wa Hospitali ya Karatu huku akisisitiza wananchi kuacha tabia ya  kuvamia maeneo ya Hifadhi na kushirikiana  na  majangili katika kuvunja sheria baadala yake washirikiane  na wahifadhi ili kutunza  maliasili kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye.

“Ndugu zangu nawasihi sana tutunze mazingira yetu, tusipotunza tunakuwa tunajiangamiza wenyewe”. Amesisitiza, Mhe. Mpango

Aidha, amewasihi wananchi waache tabia ya kujenga kwenye  shoruba za Wanyama hao  na kung’ang’ania  kuvamia hifadhi badala yake  waondoke kupisha  hifadhi kwa kuwa Tanzania imebarikiwa  kuwa na maeneo mengi ambayo yanafaa  kwa kuishi kama ambavyo  baadhi ya wananchi wa Ngorongoro walivyoamua kwa hiari yao kuondoka  kwenda kuishi Msomela Tanga  kupisha uhifadhi.

Ametoa wito kwa  viongozi wa dini, vyama vya siasa na wabunge kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi huku akiitaka hifadhi  kuboresha  mifugo na malambo ya kunyweshea  mifugo yanayozunguka hifadhi hiyo.

Katika hatua  nyingine  ameielekeza Wizara  ya maliasili na Utalii  kushirikiana na  vyuo vikuu vya hapa nchini  kufanya utafiti wa kina kuhusu  mimea  vamizi kwenye  hifadhi ili kufa na  suluhisho la changamoto hiyo.

Akimkaribisha Makamu wa Rais kutoa  hotuba yake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia na kutoa fedha za kufanyika kwa ujenzi huu wa Jengo la kisasa la ofisi.


Mhe. Mchengerwa amesema Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inatekeleza majukumu yake kwa kufuata Mpango Mkakati wa miaka mitano (5) 2020/21 - 2025/26. unazingatia mpango mkakati wa Serikali wa miaka mitano, mpango mkakati wa Wizara ya Maliasili na Utalii (2020/21 - 2025/26) pamoja na ilani ya chama Tawala (CCM) na miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali mara kwa mara.

“Mhe. Makamu wa Rais, Malengo makuu ya kimkakati ni pamoja na kuongeza idadi ya wageni kutoka wageni 700,000 mwaka 2018/19 mpaka wageni 1,200,000 ifikapo mwaka 2025/26. Kuongeza makusanyo ya mapato kutoka TZS 148 bilioni mwaka 2018/19 kabla ya UVIKO 19 mpaka TZS 260 ifikapo mwaka 2025/26. Maeneo mengine ni pamoja na kuimarisha ulinzi wa maliasili na malikale, kudhibiti janga la magugu vamizi ndani ya Hifadhi.” Amefafanua


Amesema mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya TZS TZS 10,474,526,694.25. umefikia katika kiwango cha asilimia 35 na unategemewa kukamiika mwezi Oktoba 2023, ambapo ametaja baadhi ya faida  zitakazopatikana  baada ya kukamilika kuwa ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa shirika, kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na utoaji huduma kwa wateja, kupunguza shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi.

 Aidha, kuhusu kuendelea kutoa elimu, Mhe. Mchengerwa amesema Wizara inajipanga kupitia vyuo vya usimamizi wa wanyama pori (MWEKA) na chuo cha usimamizi wa misitu (FTI), kuona uwezekano ya kuandaa program mbalimbali ya utoaji wa elimu ya uhifadhi kwa wananchi ili kupunguza changamoto  ambazo pengine zinatokana na uelewa mdogo wa wananchi.

Pia akiwa katika ziara yake mkoani leo mkoani Arusha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amefungua Hoteli ya kisasa ya hadhi ya nyota tano ya Ngorongoro O’ldeani Mountain Lodge yenye uwekezaji wa shilingi bilioni 12 iliopo Karatu mkoani Arusha inayomilikiwa na kundi la Wellworth Hotel and Lodges.
Share To:

Post A Comment: