Na John Walter-Manyara

Serikali na wadau wa Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania ( SMAUJATA) wilaya ya Babati mkoani Manyara wamesema familia zikiamua kuacha kusuluhisha Kinyumbani vitendo vya ukatili wa kijinsia, tatizo hilo litapungua na hatimaye kumalizika kabisa.

Utafiti unaonesha kwamba asilimia 60 ya ukatili kwa watoto  unafanyika nyumbani ambapo ndugu na jamaa wa karibu wanatajwa kuhusika na asilimia 40 nje ya familia ikiwamo mashuleni.

Viongozi hao wamezungumza hayo katika Kata ya Dareda wilayani Babati mkoani hapa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia Duniani inayofanyika kila mwaka Mei 15.

Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Manyara Hadija Muwango amesema wazazi wengi wanakosa demokrasia ya malezi na ubabe uliokithiri jambo linalopelekea kujenga hofu kwa mtoto na kushindwa kujiamini hata anapoanza kujitegemea na hata kufanya maamuzi yasiyo sahihi.

Katibu msaidizi SMAUJATA Mkoa wa Manyara Rest George Chuhila amesema wakati wa kufumbumbia mamcho mila na desturi zilizopitwa na wakati ni sasa hivyo jamii iache uoga katika kuripoti matukio ya ukatili yanayofanywa kwenye jamii kwa kufika vituo vya polisi au kwa kupiga 116 bure.

Katika majadiliano juu ya malezi na makuzi ya watoto na mmomonyoko wa maadili yaliyoshirikisha viongozi wa dini, mila, wazazi, walezi na Watoto, yaliyofanyika ukumbi wa chuo cha VETA Dareda,  jamii ya Wairaq walikiri tabia za ukeketaji zimepitwa na wakati na kwamba wameziacha.

Kwa upande wake afisa ustawi wa Jamii Halmashauri ya wilaya ya Babati January Bikuba amesema Madhumuni ya Siku ya Familia Duniani ni kuhamasisha, kuhimiza, kuelimisha na kutanabahisha jamii kuhusu umuhimu wa familia katika jamii kwa nia ya kuchukua hatua zinazopasa ili kuziimarisha na kuziendeleza.

Kauli mbiu ya Siku ya Familia mwaka huu ni "Imarisha Maadili na Upendo kwa Familia Imara".



Share To:

Post A Comment: