Na John Walter-Manyara

Wazazi na walezi wametakiwa kuwapeleka Watoto wao wenye umri chini ya miaka mitano kupata chanjo kwenye vituo vilivyopo katika maeneo yao ili kuwakinga na magonjwa mbalimbali.

Wito huo umetolewa na Mganga mkuu wa serikali Profesa Tumaini Nagu wakati akizundua wiki ya chanjo leo mkoani Manyara katika uwanja wa Kwaraa  mjini Babati.

Profesa Nagu amesema licha ya serikali kugharamia chanjo hizo lakini bado kuna Watoto hawajakamilisha ratiba za chanjo.

Tanzania kwa kushirikiana  na washirika wa chanjo imendaa  kampeni ya wiki ya chanjo ambayo itawalenga watoto wote walio chini ya umri wa miaka 5 ambao walikosa dozi zao za chanjo muhimu kwa afya zao ambayo imeanza leo April 24 hadi April 30 mwaka huu nchi nzima.

Kauli mbiu ya wiki ya chanjo mwaka huu inasema Tuwafikie watu  wote kwa Chanjo ikisisitiza umuhimu wa Watoto kupatiwa chanjo zote zinazostahili pindi mtoto anapozaliwa.

Mwakilishi wa WHO Boniphace Makelemo anasema UVIKO 19 imesababisha Watoto wengi kukosa huduma za chanjo hivyo ni wakati wa wazazi Pamoja na walezi kuwapeleka Watoto wao kupata chanjo.

Katika salamu zake Mwakilishi mkazi wa shirika la Afya Duniani  ofisi ya Tanzania Dkt. Zabron Yoti zilizowasilishwa kwa niaba na Boniphace Makelemo kwenye uzinduzi wa wiki ya Chanjo Kitaifa katika mji wa Babati mkoani Manyara April 24,2023, wameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua nyingi na thabiti zinazochukuliwa kupunguza athari za magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

WHO imesema Kampeni hii ya wiki ya chanjo inaonyesha dhamira ya Tanzania kulifikia lengo la kuwa na watu wanaoishi maisha marefu na yenye afya bora ambalo ni sehemu ya kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Katibu tawala mkoa wa Manyara Karolina Mthapula amesema wataendelea kuhamasisha wazazi na walezi  katika maeneo yote ya mkoa huo kuhakikisha wanawapatia Watoto wao chanjo.

 

Share To:

Post A Comment: