Na, Imma Msumba : Monduli

Maji ni rasilimali muhimu sana kwa maisha ya binadamu na wanyama, lakini katika wilaya ya Monduli, Tanzania, wafugaji na wanafunzi katika shule wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji safi na salama. Wilaya ya Monduli inapatikana kaskazini mwa Tanzania na ina eneo la kilomita za mraba 6,993.

 

Wilaya ya Monduli ni moja kati ya wilaya Saba za Mkoa Mkoa wa ArushaWafugaji wa Monduli wanategemea kwa kiasi kikubwa ufugaji wa ng'ombe, mbuzi, kondoo na punda. Wengi wao hutegemea ufugaji kama chanzo kikuu cha kipato na chakula. Hata hivyo, changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa maji ya kutosha kwa ajili ya mifugo yao na matumizi mengine ya kila siku.

 

Pamoja na hilo, ukosefu wa maji katika wilaya ya Monduli una athari mbaya kwa sekta ya elimu, ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika wilaya hii. Baadhi ya shule zimekuwa zikikabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya kila siku, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vyoo na kuosha mikono.

 

Wanafunzi katika shule hizi wanalazimika kutumia muda mwingi kusaka maji, ambayo mara nyingi huwa hayana ubora wa kutosha na hivyo kuongeza hatari ya magonjwa. Pia, wanafunzi hulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji, ambayo huathiri muda wao wa kujifunza na hata kusababisha kukosa masomo.

 

Kwa upande mwingine, hali hii ya ukosefu wa maji safi na salama katika shule pia ina athari mbaya kwa afya na ustawi wa wanafunzi. Wanafunzi ambao wanakabiliwa na ukosefu wa maji safi na salama wanaweza kupata magonjwa ya tumbo, kuhara, na magonjwa mengine yanayohusiana na uchafuzi wa mazingira.

 

Neema Mollel ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Nanja, wilayani humo, na yeye ni miongoni mwa wanafunzi wanaokabiliwa na changamoto hii.

 

Neema ameeleza kuwa maji ya kuogea na kufulia shuleni kwao wanapata kupitia mabwawa ambayo si salama, na wanapokuwa hayapatikani, wanafunzi hulazimika kutembea umbali mrefu kwenda kufuata maji kwenye bwawa la kijiji ambalo hutumiwa na zaidi ya vijiji nane. Hali hii inawafanya wanafunzi kupoteza muda mwingi kutafuta maji badala ya kujifunza, na pia kuongeza hatari ya magonjwa.

 

Hali hiyo inawaathiri sana wasichana wakati wa hedhi, ambapo wanakosa maji safi na salama kwa ajili ya kujisafisha. Wanatumia maji ya mabwawa ambayo hayawekwi dawa wala kuchujwa, na hii inaongeza hatari ya magonjwa ya zinaa na maambukizi mengine. Wanafunzi hao wanapaswa kubuni mbinu mbadala kama vile kujisafisha kwa kutumia mawe au kuchana madaftari yao, hali inayowafanya kujihatarisha na maambukizi mbalimbali.

 

"Tunateseka sana unajua shida maji hapa shuleni inaishaga kipindi cha mvua tu kwa sababu tunakuwa tunakinga na kutumia kwa matumizi lakini Baada ya msimu wa mvua kuisha tunateseka sana manake tunakuwa tunafuata maji bwawani unakuta maji Ina wadudu lakini tunatumia hivyohivyo , au muda mwingine binafsi naweza kuloanisha kitambaa nijifute Ili maji hayo yasiguse ngozi yangu hakuna namna" Amesema Neema

 

Kwa upande wa maji ya kunywa mwanafunzi huyo ameeleza kuwa,maji hayo huletwa na Gari la Jeshi na hupewa Lita 5 na huambiwa kuwa yatumike kwa siku 3 hadi siku 7 kwa matumizi ya kunywa tu lakini kufua na kuoga hutumia maji ya bwawani. Hii inaendana kinyume na mwongozo unaotolewa na Taasisi ya Kitaifa ya Sayansi, Uhandisi, na Tiba ya Marekani kuwa kiwango cha kutosha cha kunywa maji kwa siku ni karibu bilauri 15.5 (lita 3.7) za maji kwa siku kwa wanaume na bilauri 11.5 (lita 2.7) za maji kwa siku kwa wanawake.

 

 "Huwa hapa shuleni gari la jeshi ndilo linatuletea maji kwa ajili ya kunywa kiasi cha lita 5 na tunaambiwa tuyatumie kwa siku 3 hadi 7 kitu ambacho kwa matumizi ya kinywa tu bado hayatoshi"alisema mawanafunzi huyo

 

"Kwa upande wa maji ya kufulia huwa tunatumia tu haya haya ya kwenye bwaaa pamoja na kuogea,kweli tunateseka na maji hatuna,maradhi pia ni mengi katika maji haya ambayo si salama kwetu."aliongeza mwanafunzi huyo.

 

Sinyati Laizer mwanafunzi wa shule hiyo pia alisema wanafunzi wa kike wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kukutana na vishawiahi wakati wa kwenda kuchotaaji ambapo wanakutana na vijana wa mtaani na kuanza kuwarubuni kwa lengo la kutaka wawe na mahusiano nao ya kimapenzi.

 

"Wakati wa kwenda kuchota maji Huwa tunakutana na vijana wataani wakiwemo waendesha boda boda ambao hutataka tuwe na mahusiano nao ya kimapenzi na tukiwakatalia huanza kutolea lugha za vitisho hali ambayo inatusabisha kupata hofu wakati wa kwenda kutafuta maji".

 

Sinyati anasema ulinzi wao ni mdogo sana na kwamba wanapata hofu ya kufanyiwa vitendo vya ukatili na vijana wa mtaani hali inayowasababisha kwenda kuchota maji kwa hofu.

 

"Usalama wetu ni mdogo tunapotoka eneo la shule kwenda kutafuta maji tunaiomba serikali iangalie namna bora ya kutusaidia ili tupate maji ndani ya maeneo ya shule tuweze kuwa salama badala ya hivi sasa ambapo tunaishi kwa hofu kubwa ".

 

Ni wazi kwamba tatizo la ukosefu wa maji safi na salama ni kubwa sana katika wilaya ya Monduli nchini Tanzania. Kwa hiyo, kuna hatua kadhaa ambazo zinaweza kuchukuliwa ili kuboresha hali hiyo, ambazo ni pamoja na:

 

Moja kuongeza juhudi za kufikisha maji safi na salama kwenye maeneo yote ya wilaya hiyo. Serikali ya Tanzania inapaswa kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya maji, visima vya maji na mabwawa katika wilaya ya Monduli ili kuhakikisha kwamba kila mwananchi anapata huduma bora ya maji safi na salama.

 

Mbili ni kuhimiza na kusaidia wafugaji kwa njia ya mafunzo na teknolojia mpya za uhifadhi wa maji. Wafugaji wa wilaya ya Monduli wanapaswa kufundishwa njia bora za uhifadhi wa maji na kuhimizwa kutumia mifumo ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji na kupunguza athari za ukame.

 

Tatu ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa matumizi sahihi ya maji na njia bora za kuyahifadhi. Wananchi wanapaswa kufahamishwa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi maji kwa ajili ya matumizi ya siku zijazo na kutumia mbinu bora za uhifadhi wa maji kama vile kuchimba mabwawa madogo, kuhifadhi maji ya mvua na kuhimiza upandaji miti.

 

Nne ni kutoa elimu kwa wanafunzi juu ya afya na usafi wa mazingira. Wanafunzi wanapaswa kupewa elimu juu ya umuhimu wa maji safi na salama kwa afya zao na ustawi wao, na kuhimizwa kufanya mbinu bora za kujisafi na kuzuia magonjwa.

 

Tano ni kuwekeza katika teknolojia za kisasa za usambazaji na uhifadhi wa maji. Serikali na wadau wengine wanapaswa kuwekeza katika teknolojia za kisasa kama vile upandaji miti, uhifadhi wa maji ya mvua na matumizi ya mifumo ya umwagiliaji ili kupunguza athari za ukame na kuongeza uzalishaji wa mazao.

 

Kwa kuzingatia hatua hizo, tunaweza kufanya maendeleo makubwa katika kuboresha hali ya upatikanaji wa maji safi na salama katika wilaya ya Monduli, na kuboresha afya, ustawi na maisha ya wananchi wote.


Share To:

Post A Comment: